Friday, January 15, 2021

BITEKO APONGEZA KAMPUNI YA FRANONE KWA KUWA NA MGODI WENYE MIUNDOMBINU BORA


**********************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko ameupongeza uongozi wa mgodi wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd inayochimba madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Kwenye machimbo ya Tanzanite, mgodi wa Franone maarufu kama kwa Onee, unaongoza kwa kuwa na miundombinu bora kabisa ya uchimbaji.
Akizungumza baada ya kufika kwenye mgodi huo, Biteko alimpongeza mmiliki wa mgodi huo wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd Onesmo Mbise (maarufu kama Onee) kwa kuwekeza miundombinu bora ya uchimbaji.
Amesema kupitia mgodi huo imedhihirisha hata watanzania wenyewe wanaweza kuwekeza kwenye machimbo ya migodi bila kutegemea wawekezaji kutoka nje ya nchi.
“Nawapongeza kwa ujenzi mzuri wa miundombinu ya mgodi huu wa mfano kwenye machimbo ya Tanzanite hivyo wengine nao waige mfano,” amesema.
Mmiliki wa mgodi huo wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd Onesmo Mbise (maarufu kama Onee) amesema kampuni hiyo imetumia shilingi bilioni 3 hadi kukamilisha miundombinu ya mgodi huo mpya.
“Mara baada ya kuona tunataka kuboresha mgodi wetu tukiamua kuchimba kitaalamu kwa kuanzisha shaft (mgodi) mpya ambao kupitia miundombinu iliyopo shughuli za uchimbaji zinakuwa rahisi,” amesema Mbise.
Mjiolojia wa kampuni hiyo, Vitus Ndakize amesema mgodi huo umechimbwa upya kwa kilomita 1.5 hadi kukutana na mgodi wao wa awali uliopo kitalu D.
“Hata kampuni ya TanzaniteOne haina mgodi wenye miundombinu bora na ya kisasa kama hii ya kwetu japokuwa hii ni kampuni ya kizalendo,” amesema Ndakize.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amesema uongozi wa mgodi huo umechangia kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema Mbise ni miongoni mwa vijana wazalendo waliowekeza rasilimali zao kwa ajili ya kuchimba kitaalamu madini hayo.

 

No comments :

Post a Comment