**********************************************
Mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka 2021, kulitolewa taarifa ya vifo vya samaki aina ya sangara katika Ziwa Victoria nchini Uganda, hasa katika maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo
. Samaki waliokufa katika tukio hili ni aina ya sangara wakubwa.Baada ya kupata taarifa hizi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na Taasisi yake ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kituo cha Mwanza iliwasiliana na maafisa uvuvi, wavuvi, na wadau wengine wa uvuvi katika Ziwa Victoria eneo la Tanzania, kikiwemo Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU). Ufuatiliaji wetu umeonyesha kuwa upande wa Tanzania, vifo hivi havijaripotiwa sehemu yoyote isipokuwa kwa wavuvi na wananchi wa eneo la Masonga – Sota, Tarime ambao walidai kuona vifo vya samaki siku ya Jumamosi tarehe 2, Januari 2021. Hata hivyo maafisa uvuvi wa eneo husika hawakuona samaki waliokufa katika siku iliyotajwa na hata baada ya siku chache zilizofuatia. Maeneo mengine yote ya ziwa upande wa Tanzania hakukuwa na taarifa za vifo. Maeneo hayo ni Malei mpakani na Uganda, Bukoba, Misenyi, visiwa vya Ukerewe na Gozba, Busekela – Musoma, Nyamikoma – Busega na maeneo ya Mwanza na Muleba.
Aidha, katika kufuatilia jambo hili, tuliwasiliana na wenzetu wa Idara ya Uvuvi nchini Uganda ambao walituarifu kuwa walipeleka sampuli za samaki waliokufa katika maabara mbalimbali nchini mwao ili kujua kama kuna matumizi ya sumu ya aina yoyote ambayo yangesababisha vifo vya samaki ziwani. Idara ya Uvuvi nchini humo imetuhakikishia kuwa samaki hawakuwa na sumu na inadhaniwa kuwa vifo hivyo vimetokana na tukio la kila mwaka linalotokana na mchanganyiko wa maji ziwani kati ya tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni na lile tabaka la juu.
Katika Ziwa Victoria mzunguko wa majira ya mwaka husababisha matukio makubwa mawili ambayo ni: (1) utengenezaji wa matabaka ya maji kati ya tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni na lile tabaka la juu lenye hewa ya Oksijeni ya kutosha (stratification; Januari – Aprili) na (2) mchanganyiko wa maji (lake mixing) kati ya tabaka la juu na chini ambao hutokea wakati wa mvua kubwa na upepo mkubwa (Agosti – Disemba). Katika hali ya kawaida, Sangara huishi katika maji ya tabaka la kati na juu (15-20 m) ambalo lina hewa ya kutosha ya Oksijeni, yaani zaidi ya miligramu 3 kwa lita (>3mg/L). Wakati wa kipindi cha mchanganyiko wa maji, maji kutoka tabaka la chini lenye hewa ndogo ya Oksijeni hupunguza kiwango cha hewa ya Oksijeni (chini ya miligramu 3 kwa lita) katika tabaka la kati na juu wanakoishi sangara. Chini ya kiwango hiki cha hewa, Sangara, hasa wakubwa, hushindwa kuvumilia na kufa katika tukio hili maarufu kama ‘kiferezi’ au ‘fishkills’. Hali hii imekuwa ikitokea kila mwaka au kila baada ya miaka michache tangu miaka ya 1930.
Pamoja na kuwa vifo hivi havijaonekana kwenye maji ya upande wa Tanzania, kuna uwezekano kuwa mchanganyiko wa maji (mixing) unaweza kutokea kwetu pia hasa kama hali ya hewa itaruhusu wakati wa mvua kubwa na upepo. Hivyo, wizara na wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaendelea kufuatilia uwezekano wa kujitokeza vifo hivi. Pale vitakapojitokeza hatua za haraka zitachukuliwa ili kubaini kama vinasababishwa na chanzo kilichozoeleka cha mabadiliko ya hali ya ziwa au vinatokana na shughuli za kibinadamu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
No comments :
Post a Comment