Wednesday, December 9, 2020

WIZARA YA KILIMO NA GIZ KUSHIRIKIANA KUONGEZA THAMANI YA ZAO LA MPUNGA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo na Ushirikiano la Ujerumani (GIZ) Dkt. Mike Falke wakati wa kusaini makubaliano ya kuimarisha uzalishaji wa zao la mpunga kwenye mnyororo wa thamani halfa iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara Jijini Dodoma jana.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akizungumza wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano na Shirika la GIZ la Ujerumani na Taasisi ya Kilimo Trust kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akibadilishana nakala ya mkataba wa mashirikiano na Mkurugenzi wa taasisi ya Kilimo Trust Bi. Mary Shetto (kushoto) unaolenga kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akibadilishana nakala ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi Mkazi wa GIZ Dkt. Mike Falke (kushoto) unaolenga kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga kwenye mnyororo wa thamani.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( wa toka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo na Ushirikiano la Ujerumani (GIZ) mara baada ya halfa ya kusaini makubaliano ya kuongeza uzalsihaji zao la mpunga jijini Dodoma jana.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo).
****************************************

 

Serikali imengia makubaliano na shirika  la Kimataifa la Maendeleo na Ushirikiano la

Ujerumani (GIZ) kuboresha kilimo cha mpunga kwenye mnyororo wa thamani.

Makubaliano hayo yamesainiwa jana kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya na Mkurugenzi Mkazi wa GIZ Tanzania Dkt. Mike Falke jijini Dodoma na kushuhudiwa na menejimenti ya wizara pamoja na shirika la Kilimo Trust litakalotekeleza mradi huo.

Kusaya alisema makubaliano hayo yataboresha kilimo cha mpunga kwenye mnyororo wa thamani kwa kuimarisha uzalishaji,uchakataji na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mpunga.

“Tutashirikiana na GIZ ili tuwe na utoshelevu wa mpunga nchini ambapo msisitizo ni kuongeza thamani ya mpunga ili tuwe na mchele bora utakaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la nje” alisisitiza Kusaya.

Katibu Mkuu huo wa kilimo aliongeza kusema serikali ya awamu ya tano imeshatoa maagizo kwa wizara kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula na kuacha kutegemea kuagiza chakula toka nje.

Kadhalika Kusaya alibainisha kuwa makubaliano hayo yamejikita katika kuwezesha mkulima kuzalisha mpunga kwa wingi na ubora na kisha kuwezesha viwanda kupata malighafi ya kuchakata mchele hali itakayokuza ajira na uhakika wa kipato kwa mkulima na taifa.

“Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekusudia kuzalisha ajira milioni 8 hivyo kupitia zao la mpunga wizara kwa kushirikiana na GIZ na Kilimo Trust tumelenga kuongeza uzalishaji zaidi na kusaidia wakulima kupata masoko ya uhakika” alisisitiza Kusaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Kilimo Trust litakalotekeleza makubaliano hayo Mary Shetto alisema mradi huo umelenga kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga kwa kutoa mafunzo kwa wakulima, masoko,mikopo na pembejeo.

Shetto aliongeza kusema Kilimo Trust inatekeleza mradi wa kuongeza ushindani wa zao la mpunga (yaani CARI) tangu mwaka 2014 ambapo awamu ya pili ilianza mwaka 2018 na jumla ya wakulima 44,000 wamenufaika awamu ya kwanza.

“Mradi umefanikiwa kuwafikia wakulima 44,000 awamu ya kwanza na wakulima 36,000 awamu ya pili wataunganishwa na masoko ya uhakika kupitia wasindikaji wa mpunga kwenye mikoa nane ” alisema Chetto.

Shetto alitaja mikoa ya Mbeya, Songwe, Shinyanga, Tabora, Singida, Pwani, Morogoro na Iringa kuwa inatekeleza mradi huu wa kuongeza ushindani wa zao la mpunga  ambapo msisitizo ni kuzalisha mpunga bora na kuchakata kupata masoko ya uhakika ya mchele.

Kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga awamu ya pili (National Rice Development Strategy Phase II – NRDS II) uliozinduliwa mwaka 2019 Wizara ya Kilimo na wadau wanalenga kuongeza uzalishaji mpunga  kutoka tani 2,219,628 kwa mwaka 2018 na kufikia tani 4,500,000 ifikapo mwaka 2030. 

 

No comments :

Post a Comment