Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akisalimiana na baadhi wa Wafanyakazi wa Ranchi ya Kongwa muda mfupi baada ya kufika katika Rachi hiyo kukagua hali ya mifugo kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Mapafu iliyowapata baadhi ya ng'ombe katika Ranchi hiyo Iliyopo jijini Dodoma Disemba 11, 2020. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Wa kwanza kushoto) akiongea na baadhi ya Wafanyakazi wa Ranchi ya Kongwa alipofanya ziara ya kukagua hali ya mifugo kufuatia mlipuko wa Homa ya mapafu iliyowapata baadhi ya ng'ombe katika Ranchi hiyo iliyopo jijini Dodoma Disemba 11, 2020. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akimsikiliza Daktari wa Mifugo wa Ranchi ya Kongwa, Dkt. Nickson Mbise (kushoto) alipofanya ziara ya kukagua hali ya mifugo kufuatia mlipuko wa homa ya mapafu iliyowapata baadhi ya ng'ombe katika Ranchi hiyo iliyopo jijini Dodoma Disemba 11, 2020. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Daktari wa Mifugo wa Ranchi ya Kongwa, Dkt. Nickson Mbise (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) kuhusu hali ya ng'ombe baada ya mlipuko wa homa ya mapafu ulioikumba Ranchi hiyo iliyopo jijini Dodoma Disemba 11, 2020. Kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemuagiza Kaimu Meneja Mkuu, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Maselle Shilagi kuhakikisha anawapa chanjo Ng’ombe wote katika Ranchi 14 za Taifa ili kuwakinga na ugonjwa wa homa ya mapafu ulioanza kuathiri baadhi ya Ng’ombe katika Ranchi ya Kongwa.
Ndaki alitoa agizo
hilo Disemba 11, 2020 alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ranchi ya
Kongwa iliyopo Mkoani Dodoma baada ya kupata taarifa ya mlipuko wa
ugonjwa wa homa ya mapafu katika Ranchi hiyo.
Alisema kwasababu
ugonjwa huo umekuja kwa ghafla hakuna haja ya kusubiri jitihada za
haraka zichukuliwe kuudhibiti mapema kabla haujasambaa katika maeneo
mengine na kusababisha madhara makubwa zaidi.
“Kwa kuwa tayari
tuna dozi 9500 za chanjo ambazo zimefika hapa, namuagiza Kaimu
Mkurugenzi ahakikishe anaanza kuwapatia chanjo ng’ombe hawa kuanzia leo
na kufika kesho saa saba mchana nipate taarifa ya maendeleo ya uchanjaji
kwa sababu ni jambo la dharura hivyo hatuwezi kusubiri sana, ili kama
kuna mabadiliko mengine tuweze kuona ni hatua gani zinachukuliwa,”
alisema Ndaki
Aliongeza kwa kusema kuwa hali ya ng’ombe katika
ranchi hiyo bado ni nzuri na wakianza kupewa chanjo leo ugonjwa huo
utadhibitiwa huku akiwataka kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo
kuchanja ng’ombe wote waliopo katika Ranchi nyingine ili ugonjwa
usiathiri afya za mifugo.
“Nafahamu kuwa katika hizi Ranchi pia
wapo ng’ombe wa wafugaji binafsi, natoa maelekezo kuwa ng’ombe hao pia
wapatiwe chanjo pamoja na ng’ombe wa maeneo ya jirani kwa sababu
tukichanja ng’ombe wa kwetu tukaacha hao wengine tutakuwa hatujatibu
tatizo,” alisisitiza Ndaki
Aidha, Ndaki alitumia fursa hiyo
kuwaondoa hofu wafugaji wote waliopo katika maeneo ya Kongwa na sehemu
nyingine kuwa wasiwe na wasiwasi kwa sababu serikali imeshaleta chanjo
na zoezi la uchanjaji litaanza mara moja kudhibiti ugonjwa huo.
Kwa
upande wake, Daktari wa Mifugo, Ranchi ya NARCO Kongwa, Dkt. Nickson
Mbise alisema toka ugonjwa huo ulipoanza kuathiri Wanyama mpaka sasa
wameshakufa ng’ombe watano (5) kati ya ng’ombe 9200 waliopo katika
ranchi hiyo huku akisema chanzo kikubwa cha vifo hivyo ni homa ya
mapafu.
“Dalili za mwanzo tulizoziona ni ng’ombe kupumua kwa
shida na wakati mwingine ng’ombe anakimbia hovyo kama ana kichaa, na
tatizo lilivyoanza tulipata vifo vya ghafla vya ng’ombe wawili katika
mazizi tofauti, tulipowachunguza tuligundua mapafu yao yalikuwa
yameharibika hivyo tukagundua kuwa ni ugonjwa wa mapafu,” alisema Dkt.
Mbise
Aliongeza kuwa ugonjwa huo umekuwa ukisumbua sana katika
eneo hilo ndio maana huwa wanachanja mifugo mara mbili kwa mwaka, kila
baada ya miezi sita lakini kwa wakati huu ugonjwa umelipuka ghafla hivyo
wameshaagiza chanjo kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kwa
ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel
alisema kuwa atayasimamia maagizo yote aliyoyatoa Waziri na kuhakikisha
yanatekelezwa kama alivyoagiza huku akisema kuwa kufuatia maagizo hayo
wameshaleta katika Ranchi hiyo dozi za chanjo 9500 kwa ajili ya kuchanja
ng’ombe hao.
No comments :
Post a Comment