Saturday, December 12, 2020

WADAU WAKUTANA KUIMARISHA UWEZO WA UPANGAJI NA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA MAJI

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Mhandisi Dorisia Mulashani akizungumza na wadau wanaotekeleza mradi wa (WSSP II) katika kikao kazi kinachofanyika katika ukumbi wa NSSF Morogoro.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Mhandisi Dorisia Mulashani (aliyeka katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wanaoshiriki kikao kazi.

Washiriki wa kikao cha wadau wanaotekeleza mradi wa (WSSP II).

**************************************

Watekelezaji wa Mradi wa (WSSP II) ambao unalenga kuimarisha uwezo wa upangaji na

usimamizi wa rasilimali za maji, wamekutana mjini Morogoro katika kikao kazi cha kujadili mikakati ya uboreshaji wa utekelezaji wa Mradi kwa Awamu ya Pili (Second Water Sector Support Project – WSSP II).

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Mhandisi Dorisia Mulashani amesema kikao hicho ni muhimu kwani kinawakutanisha wadau muhimu na kuwapa fursa ya  kujadili kwa kina hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi na kubaini changamoto zilizojitokeza ili kuzifanyia kazi na hatimaye kuwapatia wananchi huduma ya majisafi na salama.

“Wizara ya Maji inatambua umuhimu wa kila mdau wa sekta ya maji hivyo ni matarajio yetu kuwa makubaliano na mapendekezo yatakayotolewa yatawezesha kufanikisha kufikia malengo ya mradi,” Mhandisi Dorisia amesema.

Ameongeza kuwa ana matumaini makubwa kutoka kwa wadau ambao wanatekeleza mradi huu kuchanganua na kubadilishana mawazo na pia kupata mipango mizuri inayotekelezeka na itakayowezesha kufikia malengo ya mradi na sekta ya maji kwa ujumla.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji inatekeleza Mradi wa Awamu ya Pili wa kusaidia Sekta ya Maji (Second Water Sector Support Project – WSSP II) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.

Malengo makuu ya mradi ni kuimarisha uwezo wa upangaji na usimamizi wa rasilimali za maji, kuboresha upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira katika maeneo ya kihuduma ya Dar es Salaam ambapo mradi umejikita zaidi kwenye mkoa wa Dar es Salaam.

Thamani ya mradi ni Dola za Kimarekani milioni 230, ambapo Dola milioni 225 zinatoka Benki ya Dunia na Dola milioni 5 ni mchango wa Serikali ya Tanzania.

No comments :

Post a Comment