Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye pia ni Rais wa
Baraza la Mawaziri la OACPS wakati alipokuwa anawasilisha hotuba yake
katika Mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU na
Mkutano wa 111 wa Baraza la Mawaziri kutoka nchi za Jumuiya ya OACPS
uliofanyika jana kwa njia ya Mtandao (Video Conference) jijini Dar es
Salaam.
"Kutokana na jukumu langu kama Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya
OACPS nimehutubia kwa njia ya video Bunge la pamoja la Ulaya na ACP
(ACP-EU Joint Parliamentary Assembly). Katika hotuba yangu nimehimiza
umuhimu wa mataifa makubwa kuendelea kuzifutia madeni nchi za OACPS
zilizoathiri na janga la COVID-19, pamoja na kuyataka mataifa hayo
kuhakikisha kwamba chanjo ya COVID-19 itakayopatikana inazifikia nchi
zote za Jumuiya yetu ya OACPS," Amesema Prof. Kabudi
Halikadhalika, Prof. Kabudi ameelezea hatua iliyofikiwa na nchi za OACPS
ikiwemo Tanzania katika kujenga democrasia, uchumi, biashara na
maendeleo ya watu ikiwemo suala la kulinda na kuheshimu haki za
binadamu. Aidha, aliwajulisha juu ya changamoto zinazozikabili nchi za
OACPS katika kutimiza adhma yao ya maendeleo, ikiwemo janga la ugonjwa
wa COVID -19, mabadiliko ya tabia nchi, ugumu wa kuyafikia masoko ya
ulaya, masuala ya amani na usalama ikiwemo suala la wakimbizi.
Kwa upande wake Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dkt. Gerd
Muller, ambaye pia ni Raisi wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Ulaya
alimhakikishia Prof. Kabudi kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendeleza
ushirikiano wake na nchi za OACPS katika kuhakikisha kuwa uchumi wa
Jumuiya hiyo unazidi kuimarika.
"Naomba kutumia fursa hii kukuhakikishia kuwa sisi ka EU tupo tayari
kushikamana na Jumuiya ya OACPS kuimarisha uhusiano wetu kiuchumi,
kisiasa, kidiplomasia lakini pia kulinda na kuapa kipaumbele masuala
yote yanayohusu haki za binadamu," Amesema Dkt. Muller.
Mbali na Dkt. Muller wengine waliohutubia katika mkutano huo ni pamoja
na Jutta Urpilanen, Kamishna wa Ubia wa Kimataifa kutoka EU ambaye nae
pia alisisitiza kuendeleza mshikamano baina ya nchi za EU na OACPS.
Katika hatua nyigine, Prof. Kabudi ameeleza kuwa kumalizika kwa mkutano
wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU kumetoa fursa ya
kufanyika kwa mkutano wa wa Baraza la Mawaziri wa nchi za OACPS
unaotegemewa kuanza kufanyika kwa njia ya mtandao (Video Conference)
kuanzia tarehe 13 hadi 17.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika mkutano huo, masuala muhimu yatakayo
jadiliwa ni pamoja na Mapambano dhidi ya ugonjwa Corona, majadiliano ya
mkataba mpya wa ubia mpya baina ya nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya,
Mageuzi (reforms) ndani ya Sekretariati ya OACPS, kusimamia kusainiwa
kwa Mkataba ulioboreshwa wa Georgetown (the Revised Georgetown
Agreement) na nchi za OACPS pamoja na Mikakati ya kufanya shughuli za
Jumuiya ziguse zaidi Maisha ya wananchi.
Itakumbukwa kuwa Agosti 1, 2020 Tanzania ilikabidhiwa jukumu la kuongoza
Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) kwa ngazi ya
Mawaziri na kwa ngazi ya balozi Brussels.
Jukumu hilo ni heshima kubwa kwa Tanzania na ni ishara ya wazi ya
jumuiya ya kimataifa kutambua kazi kubwa anayofanya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ndani ya nchi na
hivyo kutamani pia ushawishi wake huo uwe katika ngazi ya kimataifa
hususan katika jumuiyan hii ya OACPS.
Hii ni mara ya tatu Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hii
tangu ilipoanzishwa mwaka 1975. Tanzania ilikuwa Mwenyekiti mwaka 1992
na mwaka 2014. Chini ya Uongozi wa Tanzania vipaumbele vikuu ni pamoja
na kupambana na ugonjwa wa corona na athari zake, kusimamia
kukamilishaji wa majadiliano ya mkataba mpya wa ubia kati yan chi za
OACPS na Umoja wa Ulaya, kusimamia mageuzi makubwa ndani ya Jumuiya ya
OACPS ili iendane na wakati na kuelekeza rasilimali zake kwenye maeneo
muhimu yenye tija kwa wanachama.
Aidha, Tanzania pia imelenga kuimarishaji ushiriano miaongoni mwa nchi
za OACPS (Connectivity) na kufanya mashauriano na wabia wetu wengine wa
maendeleo ukiwemo Umoja wa Ulaya katika kuweka mifumo mizuri zaidi ya
kuimarisha biashara, ongezeko la thamani ya mazao ya kilimo, matumizi ya
digitali na fursa zaidi za masoko.
No comments :
Post a Comment