Tuesday, December 8, 2020

SHIRIKA LA POSTA LAANZISHA DUKA MTANDAO, WAFANYABISHARA 90 WAJISAJILI

Meneja wa Biashara za E-Commerce  Wa Shirika la Posta Tanzania, Amina Salum akitoa huduma kwa mteja aliyefika katika banda lao kupata huduma ya kujiunga na Duka mtandao (Posta Online shop)  na Shirika la Posta Tanzania.Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

Shirika la Posta Tanzania limewataka wafanyabiashara, wajasiriamali wa mtandao

kujisajili katika huduma ya duka mtandao (Posta Online shop) ili kuongeza wigo wa biashara zao.

Hayo yamesemwa wakati wa maonesho ya Tano  ya Viwanda yanayoendelea ndani ya Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia huduma hiyo mpya, Meneja wa Biashara za E-Commerce, Amina Salum amesema Shirika limeanzisha huduma hiyo ili kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali kufanya biashara zao kwa njia ya mtandao.

Amesema, Mteja atajisajili kwa njia ya mtandao, ataweka bidhaa zake na maelezo kama bei, uzito na akishamaliza mteja ataweza kuona bidhaa hizo kupitia duka  mtandao (Posta Online shop).

"Mteja anaweza akanunua bidhaa hizo kupitia huduma za kifedha za Tigopesa, M-pesa, Airtel Money au kwa Credit Card na Shirika la Posta litaenda kuchukua hiyo bidhaa kwa muuzaji na kuipeleka kwa mteja iwe ndani au nje ya nchi," amesema Amina

"Tunawakaribisha wafanyabishara wote waje kujisajili katika huduma hii kwani ni bure na hadi sasa jumla ya wateja 90 wameshajisajili katika huo mtandao na litazinduliwa hivi karibuni," amesema.

Aidha, Amina amesema faida kubwa ya duka mtandao (Posta Online shop)  ni kubwa wafanyabishara wa bidhaa mbalimbali watapata fursa ya kuuza bidhaa zao, kwahiyo duka hili litamsaidia mfanyabishara kuuza bidhaa zake kwa msaada wa Shirika la Posta.

Amesema, kupitia Shirika la Posta, mteja anaweza akanunua bidhaa tofauti kwa wakati mmoja na akalipia hapo hapo alipo na  atapelekewa hadi nyumbani.

Akielezea dhana inayosambaa kuhusiana na utapeli kwa bidhaa za mtandao, Amina amesema Shirika la Posta ni la kiserikali ila itakapotokea kuna hitilafu kwenye bidhaa Shirika litamtafuta muuzaji wa bidhaa ili iweze kubadilishwa na kuipeleka tena kwa mteja, Shirika  hili ni kongwe na limeenea nchi nzima.

Kwa sasa Shirika la Posta liko mbioni kuzindua huduma hiyo rasmi wakiwa na mikakati ya kuingia ubia na TanTrade ili kuwapata wafanyabishara wengine wanaouza bidhaa zao nje ya nchi.

 

No comments :

Post a Comment