Tuesday, December 8, 2020

KAMPUNI 6 ZASAINI MKATABA NA TANESCO KUZALISHA UMEME WA MAJI

Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati wa Tanesco, Eng. Costa Rubagumya  akitiliana saini mkataba na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kampuni ya Lung’ali Natural Resources, Father Luciano Mpoma inayoendesha mradi wa Maguta Hydropower  1.2MW  umeme unaozalishwa kutoka maporomoko ya maji ya Mto Lukosi, wilayani Kilolo. Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Tanesco Desemba 8, 2020. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA

Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati wa Tanesco, Eng. Costa Rubagumya  akishuhudia viongozi wa kampuni ya  Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd wakitia saini mkataba kuendesha mradi wa Ijangala Hydropower  unaozalisha umeme wa maji kutoka maporomoko ya Mto Ijangala, wilayani Makate yenye uwezo wa kuzalisha 0.36MW.

 viongozi wa  Kampuni ya Madope Hydro Company Ltd, wakitia saini mkataba wa kuendesha Mradi wa umeme wa Madope Hydropower 1.7MW, unaotokana na  maporomoko ya maji ya Mto Madope wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe. Kulia ni Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati wa Tanesco, Eng. Costa Rubagumya. Kampuni hiyo itaiuzia umeme Tanesco.

Nicholas Richardson Mkurugenzi Mtendaji wa  Kampuni ya SSI Eenergy Tanzania Ltd akisaini mkataba wa kuendesha  Mradi wa Kahama Solar Power 10.0MW utakaozalisha umeme wa jua karibu na Mgodi wa Dhahabu wa  Buzwagi wilayani Kahama. Miradi yote sita ina uwezo wa kuzalisha  megawati 19.16 zitakazouziwa Tanesco.

 

 


Viongozi wa Tanesco wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kampuni sita baada ya kutiliana saini mkataba wa kuzalisha umeme na kuiuzia

Tanesco. Hafla hiyo imefanyika  Makao Makuu ya Tanesco jijini Dodoma .

Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma

KAMPUNI sita zimeingia zimesainiana mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa kuziana umeme  wa miradi midogo ya kuzalisha umeme.

Tukio hilo limefanyika leo Desemba 8, 2020 katika makao makuu ya Tanesco jijini Dodoma ambapo kampuni hizo zitazalisha umeme wa maji  na wa jua.

Kwa upande wa Tanesco mikataba hiyo ilisainiwa na Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati wa Tanesco, Eng. Costa Rubagumya huku kila kampuni  ikiwakilishwa na viongozi wao wakuu.

Mikataba hiyo imesainiwa kwa mujibu wa kanuni zilizoidhinishwa na  Ewura na zinazosimamia  uenderezaji wa miradi midogo ya kuzalisha umeme. Kampuni binafsi zinaruhusiwa kuendeleza miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia  nishati jadidifu(maji, upepo, jua tungamotaka) katika maeneo mahsusi kwa malengo ya kuuza umeme kwa wananchi au Tanesco.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Eng. Rubagumya alisema kuwa wawekezaji ambao wanategemea kuzalisha umeme na kuuza kwa Tanesco, mikataba maalumu ya kuuziana umeme  inatakiwa kusainiwa baina ya wawekezaji husika na Tanesco.

Alisema kabla ya tukio la leo, Tanesco na Wawekezaji wa miradi sita ya kuzalisha umeme walikutana kwa lengo la  kufanya maboresho kwenye mikataba ya kuuziana umeme. Mikataba iliyofanyiwa maboresho imepata idhini ya Ewura hivyo kupata baraka ya kusainiwa.

Aidha Tanesco imezipa kampuni hizo muda wa miezi 18 kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ili ianze  kutoa huduma kwa wananchi.

Kampuni sita zilizosaini mikataba ni; Nishati Lutheran (DKK) Investment Ltd inayomiliki mradi wa Ijangala Hydropower  unaozalisha umeme wa maji kutoka maporomoko ya Mto Ijangala, wilayani Makate yenye uwezo wa kuzalisha 0.36MW.

Kampuni ya Madope Hydro Company Ltd, inayoendesha Mradi wa umeme wa Madope Hydropower 1.7MW, unaotokana na  maporomoko ya maji ya Mto Madope wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe.

 Kampuni ya Luponde Hydro Ltd,  inayoendesha mradi wa Luponde Hydropower 0.9MW  unaotoka na na maporomoko ya maji ya Mto Luhololo, wilayani Njombe.

Kampuni zingine ni; Kampuni ya Lung’ali Natural Resources inayoendesha mradi wa Maguta Hydropower  1.2MW  umeme unaozalishwa kutoka maporomoko ya maji ya Mto Lukosi, wilayani Kilolo.

Kampuni ya Nextgen Solawazi  Ltd inayoendesha mradi wa  Kigoma Solar Power 5.0MW inayozalisha umeme wa jua eneo la Kigoma Special; Economic Zone.

Kampuni ya SSI Eenergy Tanzania Ltd ya Mradi wa Kahama Solar Power 10.0mw, umeme wa jua karibu na Mgodi wa Dhahabu wa  Buzwagi wilayani Kahama. Miradi yote sita ina uwezo wa kuzalisha  megawati 19.16.

 

No comments :

Post a Comment