Thursday, December 31, 2020

NFRA Wajipange kununua Mahindi mengi kwa Wakulima – RC Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyechuchumaa) akiangalia moja ya mfumo wa Kihenge kilichomalizika kujengwa katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa vihenge hivyo akiwa na timu ya wataalamu wa Mkoa na Wilaya pamoja na NFRA.

Timu ya Wataalamu wa Kilimo kutoka Ofisi ya mkuu wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa huo Mh. Joachim Wangabo wakiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa katika eneo la Viwanda la Kanondo katika Manispaa ya Sumbawanga. 

**************************************

Wakati Utekelezaji wa lengo la Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) la kuweka mfumo wa kisasa wa kutunza mazao kufikia asilimia 80. Wakala hao wameshauriwa

kujiandaa kununua mahindi mengi Zaidi ili kuwahakikishia wakulima soko la mazao yao katika kipindi cha msimu wa 2020/2021

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa ni vyema NFRA wakaongeza fedha za kununua mahindi na kisha kutafuta soko nje ya nchi hasa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Pamoja na nchi nyingine ili kuwapa fursa wakulima nchini kufanya biashara na NFRA ili kuepuka kuhangaika kutafuta soko la mazao yao.

“Mkoa wa Rukwa tumezalisha tani za mahindi tani 585,000 na matumizi yetu ya ndani ni tani 291,000 kwahiyo tulikuwa tuna ziada ya tani 294,000, sasa ukiangalia kwamba tani 294,000 halafu mahindi yananunuliwa tani 11,000 kwahiyo mahindi mengi yalibaki ndio kikawa kilio cha wakulima wa mkoa wetu wa Rukwa kwahiyo nategemea kwamba ukamilishwaji wa vihenge hivi NFRA itakuwa na uwezo wa kuchukua tani 58,500, hii kwa sisi mkoa wa Rukwa ni sawa na kuingiza na kutoa ili wawauzie watu wengine.”

“Kwahiyo niwaombe NFRA ndio wamekuwa mkombozi sasa kwa wakulima, mjipange vizuri ili kuongeza fedha muweze kununua mahindi mengi kwa wakulima vinginevyo wakulima watakata tamaa na sasa wanaendelea kuzalisha baada ya kuona kwamba hivi vihenge hapa vinakwenda kukamilika kwahiyo uwezo wa NFRA utakuwa mkubwa Zaidi wa kununua mahindi kwa wakulima, ninyi mnao uwezo wa kuona wapi muyapeleke hayo mahindi, ninyi mfanye biashara na nje na sisi tufanye biashara na nyie,” Alisema.

Kwa upande wake Mhandisi Mkazi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Haruna Kalunga amesema kuwa hadi tarehe 28.12.2020mkandarasi ameshatumia muda wake wa miezi 15 sawa na asilimia 83 ya muda aliopewa kwenye mkataba huku utekelezaji ukiwa ni asilimia 80 na hivyo kuufanya mradi kuwa nyuma kwa asilimia 3 na kuongeza kuwa ucheleweshwaji huo umechangiwa na kucheleweshwa kwa msamaha wa kodi wa vifaa vinavyotoka nje ya Tanzania.

Kwa mkoa wa Rukwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Unia Araj kutoka Poland ikisaidiana na Mkandarasi Mzawa Elerai kutokea Arusha kwa thamani ya Dola za marekani 6,019,399.00 ambayo ni asilimia 30 ya mradi mzima unaotekelezwa katika mikoa mitatu Pamoja na Mkoa wa Katavi na Manyara wenye jumla ya thamani yad ola za marekani 20,280,906.00.

No comments :

Post a Comment