Thursday, December 17, 2020

MRADI WA JIFUNZE WAWASAIDIA DARASA LA SABA WASIOJUA KUSOMA LUDEWA

Mwalimu wa darasa la Jifunze, Andrea Mhagama kutoka Shule ya Msingi Maholong'wa akiwafundisha wanafunzi wa darasa hilo maalum shuleni hapo. 
Mwalimu wa kujitolea darasa la Jifunze, Charles Habiye wa Shule ya Msingi Maholong'wa akiwafundisha wanafunzi wa darasa hilo maalum shuleni hapo hivi karibuni. 
Mwalimu wa darasa la Jifunze, Andrea Mhagama kutoka Shule ya Msingi Maholong'wa akiwa darasani na wanafunzi wa darasa hilo maalum. 
Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani).
Mwalimu Mkuu Msaidizi, Shule ya Msingi Maholong'wa, Chefasi Mdesa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani)

Na Joachim Mushi, Ludewa
MRADI maalum wa Jifunze unaotekelezwa katika baadhi ya Shule za Msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ukiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kuanzia darasa la tatu hadi la sita wasiojua kusoma na kuandika, umewasaidia wanafunzi sita wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Maholong'wa kuweza kufanya vizuri mtihani wa taifa.

Wanafunzi hao ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika kwa ufasaha walilazimika kujumuishwa kwenye darasa maalum la Jifunze lililokuwa likiendeshwa baada ya vipindi vya kawaida vya masomo kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wa kuanzia darasa la tatu hadi la sita, kwenye shule hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi wilayani hapa, Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve alisema wamefanya majaribio ya kuwaingiza watoto sita wa darasa la saba shule ya Msingi Maholong'wa, ambao walikuwa na changamoto ya kutokumudu vizuri kusoma na kuandika kwenye darasa la Jifunze bila ya kuandikishwa rasmi ikiwa ni jitihada za kuwasaidia ili waweze kufanya mitihani yao ya mwisho.

Alisema awali baada ya ukaguzi uliofanyika Mwezi Machi, 2020 katika Shule ya Msingi Maholong'wa walibaini uwepo wa wanafunzi sita wa darasa la saba wasiojua kusoma na kuandika na kuwapanga walimu kuwasaidia kwa muda wa ziada ili waweze kufanya mitihani yao ya mwisho, njia ambayo haikuzaa matunda hadi walipojumuishwa katika darasa la Jifunze na ndani ya siku kumi tu waliweza kumudu kusoma na kuandika hivyo kurejeshwa katika darasa lao na kuendelea na masomo.

"...Baada ya kuingia katika darasa hilo la Jifunze ndani ya siku 10 watoto hawa wote walimudu kusoma kwa ufasaha vizuri na wamefanya mtihani wao wa mwisho kwa shule ya msingi wakiwa wanajua kusoma na kuandika na hata baada ya matokeo yao ni mtoto mmoja tu ndio ameingia katika kundi la 'D' yaani kafanya vibaya, lakini awali tulitegemea shule hii watoto hao wote sita wangefanya vibaya na kuingia kundi 'D'," alisema Bw. Mtweve.

Aidha akifafanua zaidi alisema mradi huo wa Jifunze umewasaidia pia baadhi ya wanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Mkongobaki Wilayani Ludewa ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika kumudu masomo yao na kuleta ushindani darasani. 

"...Kuna shule nyingine ya Mkongobaki tulifanyisha mtihani wa Mock wa Wilaya nzima baadhi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wa darasa la nne wa shule ya msingi mkongobaki walikuwa wanafaulu kwa kiwango cha chini sana lakini wanafunzi hao baada ya kuingia kwenye mradi wa Jifunze walibadilika na kuanza kufanya vizuri na kuleta ushindani kwa wenzao darasani, jambo ambalo awali hawakuwa na ushindani huo," alifafanua Mdhibiti huyo wa ubora wa shule wilayani Ludewa.

Mradi wa Jifunze unaoratibiwa na Taasisi ya Uwezo Tanzania kusaidia kupunguza wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa darasa la tatu hadi la Sita umekuwa ukitekelezwa kwa baadhi ya wilaya zenye changamoto ya ujifunzaji kwa wanafunzi, na umekuwa ukiwatumia walimu kwa muda wa ziada kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto ya kutokujua kusoma na kuandika kwa ufasaha. 

Mradi umekuwa ukitekelezwa kwa walimu kutoa mada kwa vitendo na ukaribu zaidi na wanafunzi, kujenga urafiki, kutumia vifaa rahisi kufundishia, kuimba na kucheza na kutoa motisha kwa wanafunzi wanaojifunza jambo ambalo limekuwa na mabadiliko makubwa katika kujifunza kwa wanafunzi.

 

No comments :

Post a Comment