VIJANA
283 kati ya 301 waliohitimu mafunzo ya Ukarimu na Utalii mwaka 2020
katika Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VETA Njiro) jijini Arusha
wamepata ajira.
Akipokea
taarifa ya wahitimu hao katika Mahafali ya nane ya Chuo hicho
iliyofanyika jijini Arusha tarehe 4 Desemba, 2020, Afisa Tawala wa
Wilaya ya Arusha, Ndugu Nyangusi Nyailiba, aliyemwakilisha Mkuu wa
Wilaya ya Arusha, alisema takwimu hizo zinathibitisha ubora wa mafunzo
yanayotolewa na VETA na kuonyesha namna sekta ya Ukarimu na Utalii ina
uhitaji mkubwa wa rasilimali watu yenye ujuzi na weledi.
“Takwimu
hizi za wahitimu ambao wako kazini ni ushahidi wa ubora wa mafunzo
yanayotolewa na chuo chetu na juhudi hizi zinaunga mkono dira ya nchi ya
kujenga uchumi wa viwanda sambamba na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais
wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli,”alisema.
Ndugu
Nyailiba alihamasisha uongozi wa Chuo cha VETA Njiro kubuni mafunzo
zaidi na kuongeza udahili kupitia mafunzo ya muda mfupi kwenye sekta ya
hoteli na utalii ili kuweza kugusa na kubadilisha maisha ya wananchi
wengi wa jiji la Arusha wanaotegemea sekta hiyo kujiingizia kipato.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema Mamlaka itaendelea kuboresha
mazingira ya kufundishia ya chuo hicho ili kuwezesha chuo kuzalisha
wahitimu wengi zaidi wa kuhudumia sekta ya utalii yenye mchango mkubwa
kwenye uchumi wa nchi.
Alisema
Mamlaka imeanza kazi ya upanuzi wa chuo hicho ambapo kwa mwaka 2020,
kiasi cha shilingi milioni 647 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa
madarasa mawili, ukumbi wa mihadhara, maliwato pamoja na ukarabati wa
majengo ya hoteli na utawala ya chuo hicho. Ujenzi huo umeanza na
unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2021.
Awali,
Mkuu wa Chuo hicho, Ndugu Christopher Ayo, alisema wanafunzi 16
wamehitimu kwa ngazi ya stashahada, 218 Astashahada na 67 wamehitimu
ngazi ya tatu ya Ufundi Stadi (NVA Level III).
Aliwasihi
wahitimu hao kujikita zaidi kwenye eneo la kujiajiri ili waweza
kuzalisha ajira kwa vijana wengine hasa kwa kuzingatia kuwa pamoja na
mafunzo ya fani za hoteli na utalii, pia wahitimu hao walijifunza
ujasiriamali, namna ya kutafuta masoko ya bidhaa pamoja na huduma kwa
wateja .
Ayo alisema chuo hicho kimelenga kuongeza udahili kutoka wanachuo 411 kwa sasa hadi kufikia 700 ifikapo mwaka 2023.
Mmoja
wa wahitimu wa chuo hicho, Amos Julius, alisema uwepo wa hoteli ya
kisasa yenye hadhi ya nyota tatu (Three Stars Hotel) chuoni hapo mahsusi
kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi imesaidia sana wanafunzi
kuweza kufanya mazoezi kwa vitendo mara nyingi zaidi na kuwaongezea
ujasiri katika kufanya kazi kwenye sekta ya hoteli na utalii.
Chuo
cha VETA Njiro kilianzishwa mwaka 2011 na kinatoa mafunzo ya muda mrefu
katika fani za Upishi,Huduma ya Mauzo ya Vinywaji na Chakula, Usafi wa
Nyumba na Udobi, Uongozaji Watalii ,Usimamizi wa Uendeshaji wa shughuli
za Utalii, Mapokezi Huduma za Malazi na Sanaa ya Mapishi.
Chuo
pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali ikiwemo
Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi, Huduma ya uuzaji
vinywaji, uandaaji wa keki na mafunzo ya uongozaji watalii.
No comments :
Post a Comment