Sunday, December 6, 2020

MENEJIMENTI YA MKOA WA IRINGA YATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI MKOANI DODOMA

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Happiness Seneda akielezea jinsi Mkoa wa Iringa unavyonufaika na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ofisini kwake.

Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zainab Manyike akielezea fursa za uwekezaji zilizopo Jiji la Dodoma kwa Menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa

……………………………………….

Na. Dennis Gondwe, IRINGA

KATIBU Tawala Mkoa wa Iringa, Happiness Seneda ameitaka timu yake ya menejimenti

kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kauli hiyo aliitoa katika kikao cha Menejimenti cha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo mwishoni mwa wiki.

Seneda alisema kuwa amewakaribisha wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kikao cha Menejimenti ili kuelezea fursa zilizopo jijini Dodoma.  

“Serikali imefanya maamuzi mazuri kuhamishia makao makuu Dodoma kwa sababu kumefungua fursa nyingi ambazo hazikuwepo awali. Na sisi tunataka kunufaika na fursa hizo, wawekezaji wa kwanza ni sisi” alisema Seneda. Timu ya wataalam wataelezea fursa za uwekezaji zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwashawishi kuzichangamkia, aliongeza.

“Ndugu zangu hakikisheni mnawekeza Dodoma, humtajutia sababu fursa nyingi zipo wazi. Unapofanya uwekezaji jijini Dodoma maana yake, wewe unakwenda kutengeneza Masaki ya Dodoma na Posta ya Dodoma. Usije kuona kuwa Dodoma ni mbali, muda mfupi ujao utakuja kujutia. Mfano eneo la Nzuguni litakuja kupaa sana, uwanja wa mpira utajengwa hapo, kituo kikuu cha mabasi kipo Nzuguni, soko kuu la Job Ndugai lipo Nzuguni hilo ni eneo la kimkakati,” alisema Seneda.

Kwa apande wake Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zainab Manyike alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina fursa nyingi za uwekezaji. 

“Halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda mbalimbali katika Kata ya Nala. Eneo la Nala linapatikana barabara kuu ya kwenda Singida umbali wa kilometa 15 kutoka katikati ya Jiji. Eneo hili ni la kimkakati kwa ajili ya viwanda vya aina mbalimbali vikubwa na vidogo” alisema Manyike.

Akifafanua zaidi alisema kuwa maeneo yaliyotengwa ni kwa ajili ya viwanda vya kufua umeme wa upepo, matengenezo ya magari, na viwanda vya Dawa. Vingine ni viwanda vya nguo, viwanda vya vyakula, viwanda vya chuma na viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya biashara.

Aliongeza kuwa Halmashauri hiyo imepima viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama ujenzi wa hoteli na nyumba za kupangisha katika maeneo ya Mtumba, Iyumbu, Njedengwa na Kitelela. Fursa nyingine alizitaja kuwa ni ujenzi wa shule na vituo vya afya. “Wote tunafahamu kuwa Jiji linaendelea kukua kutokana na idadi ya watu kuongezeka hivyo kuna fursa za uwekezaji katika ujenzi wa shule kwa ajili ya huduma za elimu. Vilevile, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya huduma za matibabu. Viwanja kwa ajili ya matumizi ya shule na hospitali vinapatikana maeneo ya Mtumba, Kikombo, Chahwa na Nala” alisema Manyike.

Kiutawala Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina ukubwa wa kilometa za mraba 2,576, ikiwa na kata 41 na mitaa 222.

 

No comments :

Post a Comment