Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kama fursa ya
kutangaza kazi zao na kutetea haki za wanawake na watoto badala ya kutumia kwa mambo yasiyofaa katika jamii kama vile kusambaza zisizo na maadili.Rai hiyo imetolewa Novemba 20,2020 na Katibu wa Jukwaa la Vijana Wafeminia kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Zawadi Kondo kwenye Warsha ya Mtoto wa kike, Teknolojia na Ubunifu wakati wa Tamasha la 6 la Jinsia wilaya ya Mbeya katika uwanja wa kijiji cha Hatuelo kata ya Ijombe halmashauri ya Mbeya.
Kondo alisema Mitandao ya Kijamii ikitumika vizuri ni chachu ya maendeleo hivyo kuwataka vijana hususani wa kike kuacha kusambaza vitu vya hovyo mitandaoni na badala yake watumie kama fursa ya kutangaza kazi wanazofanya na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Ukitumia vizuri mitandao ya kijamii utapata faida. Naomba mtumie kwa ajili ya kujiletea maendeleo”,alisema.
Kondo alieleza kuwa Mitandao ya Kijamii imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa watetezi wa haki za wanawake na watoto kufuatilia matukio ya ukatili yalipo pindi yanaporipotiwa na kwamba inasaidia kufanya uchechemuzi.
Kwa upande, Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana Wafeminia Alphonsina Ambrose aliwataka wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao kufanya vitu wanavyopenda kufanya na kuwapeleka shule watoto wenye ubunifu ili kukuza ubunifu wao.
“Mzazi mpe nafasi mtoto afanye vitu anachokipenda akifanye kwa usahihi ilmradi viwe vitu vizuri. Mzazi asikilize maoni ya mtoto wake lakini katika kufanya hayo mzazi asiache kumpa haki ya elimu ili kuboresha ubunifu wa mtoto”,aliongeza Alphonsina.
“Hata kama mtoto ana ubunifu mkubwa kiasi gani ni lazima apelekwe shule. Elimu anayopata itamsaidia kuboresha kazi zake za ubunifu ili kumtengenezea maisha mazuri na hatimaye kujenga jamii yenye usawa”,aliongeza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi aliwasisitiza vijana na wanawake kuwa wabunifu katika kazi wanazofanya na kutumia fursa walizonazo kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja kuhakikisha wanaongeza thamani kwenye mazao wanayolima.
No comments :
Post a Comment