Mstaafu na mwenza wake wakifurahia manufaa ya kuwekeza kwenye dhamana za serikali za muda mfupi. (Picha ya mtandao)
Na Christian Gaya. Majira Ijumaa 20. Novemba. 2020
Mara nyingi wawekezaji wanaotegemewa wakiwemo hata baadhi ya wastaafu wengi, huwa hawana uhakika kuhusu ni kitega uchumi kipi kitawawezesha kupata faida kubwa zaidi baada ya kustaafu, badala ya kubaki na kutumia tu akiba za mafao yao ya mikupuo pamoja na...
pensheni zao za kila mwezi.Kwa sababu hata kulingana na utafifi uliofanywa hivi karibuni unaonesha ya kuwa idadi kubwa ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanaochukua fao la kukosa kazi na wastaafu waliofikisha umri wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima kwa mujibu wa sheria hawashiriki katika kuwekeza kwenye dhamana za serikali, hisa, na hata kununua vipande.
Pia tafiti mbalimbali zinaonesha ya kwamba zaidi ya asilimia arobaini ya watanzania hawajawahi kusikia kuhusu dhamana ya serikali, vipande na hisa huku idadi ya wanawake ikiwa ni kubwa zaidi ikiiongoza kuliko idadi ya wanaume ukilinganisha na idadi ya watanzania wote wapatao milioni 55 mpaka sasa.
Kwa sababu utafiti pia unaonesha ya kuwa zaidi ya asilimia themanini na nne (84%) ya watanzania wanahitaji elimu kuhusu jinsi ya kuweka akiba na kuwekeza, wakati asilimia themanini (80%) wanahitaji elimu ya kuthibiti na kusimamia fedha.
Mpaka kufikia mwezi Juni 2009, kati ya watanzania milioni arobaini (40m), ni asilimia sifuri nukta tisa (0.9%) ya Watanzania walishiriki katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Hiyo inamaanisha ya kuwa ni watanzania chini ya au waliozidi laki 200,000 ndio waliokuwa wanashiriki katika soko la hisa la Dar es Salaam kati ya milioni 40,000,000 mpaka kufikia mwaka 2009.
Fursa hii ya uwekezaji katika hatifungani za serikali inaonesha kutumiwa na watu wachache sana kutokana na watu wengi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kutumia chanzo hiki cha utajiri.
Hivyo basi, kuwekeza katika dhamana za serikali yaani katika hatifungani za muda mfupi zinaweza kuwa ni fursa bora zaidi yenye kueleweka na wengi na hasa kwa wafanyakazi watanzania wanaostaafu kila siku kukicha kutoka katika taasisi za umma na watu binafsi zikiwemo pamoja sekta zilizo rasmi na zisizo rasmi.
Hatifungani za muda mfupi zinaaminika ya kuwa zina fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinaweza kutoa marejesho makubwa ya uwekezaji wake kwa haraka kama zinaweza kutumiwa ipasavyo kama fursa za uwekezaji kwa wastaafu wengi ili kujiongezea kipato zaidi badala ya kutegemea pensheni ya kila mwezi ambayo wala haiendi pamoja na mfumuko wa bei wa kila mwezi.
Hivyo hatifungani za muda mfupi ni za aina ya uwekezaji zinazoaminika kwa umma kama vile wastaafu wa hiyali au wa lazima, zinazoweza kugarantia mapato ya mstaafu ya kila mwezi au mwaka kwa uhakika zaidi ukilinganisha na uwezekezaji wa vitegauchumi vingine kwa sababu aina hii ya dhamana ya serikali haina aina yoyote ya hali hatarishi.
Kwa kawaida Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza dhamana za serikali ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa taasisi na kwa mwananchi mmoja mmoja kama vile wastaafu wanaopata mafao yao ya mkupuo na pensheni zao za kila mwezi.
Hivyo basi, hati fungani za serikali ni fursa nzuri ya uwekezaji hasa kwa wastaafu wanaohitaji kuwekeza fedha na kupata faida bila kutumia nguvu nyingi au kuwekeza bila kupata hasara.
Kulingana na mwongozo wa namna ya kushiriki katika soko la awali na la upili la dhamana za serikali za muda mfupi, Benki Kuu ya Tanzania hutoa dhamana za serikali za muda mfupi na zinazoiva kwa nyakati tofauti. Dhamana hizi ni huwa ni za siku 35, 91,182 na za siku 364.
Mwongozo ufafanua zaidi ya kuwa, Dhamana za serikali za muda mfupi kwa kiwango kikubwa huiwezesha serikali kugharamia kwa muda nakisi katika bajeti yake inayosababishwa na upungufu wa mapato ukilinganisha na matumizi ya Serikali.
Hivyo basi, hatifungani za muda mfupi ni kitegauchumi chenye uhakika mkubwa kwa mfanyakazi yeyote anayetegemea kustaafu au kwa aliye staafu bila kuguswa na msongo wa mawazo kwa muda wote wa uwekezaji wake.
Kwa upande mwingine hatifungani za muda mfupi zinachoweza kutumika kujiongezea pato kimya kimya bila usumbufu wowote kwa kupata fedha na riba yake.
Hatifungani za muda mfupi ni kimiminika cha fedha, ikiwa na maana ya kuwa hatifungani ni kitu ambacho unaweza kukibadilisha kirahisi wakati wowote kupata fedha taslimu bila kupoteza riba kama faida yako itokanayo na serikali kukopa kwako wewe mstaafu.
Kwa sababu dhamana za serikali za muda mfupi pia zinafuata kanuni za usalama wa mtaji, na uwezo wa kuleta faida ya uhakika, pia hatifungani za muda mfupi ni kitega uchumi zinachoweza kubadilika kuwa fedha taslimu.
Mwongozo huo wa namna ya kushiriki unaeleza wazi ya kuwa dhamana za serikali huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani kupitia minada na baada ya hapo uuzaji wa dhamana hizo hufanywa kwenye soko la upili.
Ambapo soko la awali la dhamana za serikali ni njia ya kukopa fedha moja kwa moja kutoka kwa taasisi ama kwa mwananchi mmoja mmoja
Soko hili la awali mara nyingi linakuwa wazi kwa taasisi za fedha kama vile mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii na kadhalika, lakini mwitikio unaweza kutembelewa kwanza na wateja mbalimbali wanaotaka kuwekeza mpaka kufikia kiasi cha fulani cha fedha kupitia benki zao za biashara.
Mara nyingi tangazo hutolewa kupitia vyombo vya habari kwa ajili ya uitishaji wa zabuni na hutolewa wiki moja kabla ya siku ya mnada.
Wawakilishi wanapaswa kutumia fomu maalumu za zabuni zinazoitwa CDS/FORM/03 kwa ajili ya kushiriki katika minada ya dhamana za serikali. Fomu hizi zinapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania na katika ofisi za mawakala waliosajiriwa kama vile taasisi za fedha na mabenki mbalimbali.
Benki Kuu ya Tanzania imesajili mabenki na madalali wa soko la hisa la Dar Es Salaam kufanya kazi za uwakala kwa wawekezaji katika dhamana za serikali.
Mwongozo unataja ya kuwa kiwango cha chini cha kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali za muda mfupi ni shilingi laki tano tu (500,000) zikiwa katika mafungu ya shilingi elfu kumi kumi (10,000).
Bei ya dhamana za serikali za muda mfupi zinapaswa kuwa na tarakimu nne za desimali.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz
Inaendelea wiki ijayo
No comments :
Post a Comment