Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya fedha kwa ajili ya wanafunzi watakaonufaika na mkopo ambapo kwa mwaka huu kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 464 ambapo ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na mwaka jana.
Badru ameoongeza kuwa HESLB imeshaanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo vyao na kuwataka wanafunzi kufuatilia na kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na mikopo yao katika akaunti walizotumia kuomba mkopo unaojulika kama SIPA (Student’s Individual permanent Account).
“Serikali imeshatupia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni, lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao.”Amesema Badru
Amebainisha kuwa wanafunzi waliopata mkopo wana sifa zikiwemo kuwa wahitaji, kuomba kwa usahihi na kuwa na udahili wa chuo kimoja pia orodha ya awamu ya pili ya wanafunzi waliopangiwa mkopo imepangwa kutolewa siku ya Jumamosi Novemba 14, 2020 baada ya ya bodi ya mikopo kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea.
Aidha katika mkutano huo Badru amesema kuwa wanafunzi wenye mikopo wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wapatao 44, 629 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 155.06.
“Wanafunzi hawa 44,629 wamepangiwa mikopo baada ya HESLB kupokea matokeo ya mitihani yanayothibitisha kuwa wamefaulu kuendelea na masomo katika mwaka unaoanza , HESLB inaendelea kupokea matokeo ya wanafunzi waliokua na mikopo mwaka wa masomo uliopita na watapangiwa mikopo.” Amesema Badru
Hata hivyo Badru amewataka waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata na amewataka wanafunzi walionufaika na mkopo wa elimu ya juu kuwa waaminifu na kulipa mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kuwasaidia wanafunzi wengine wenye uhitaji.
“Mnaokopa mnapaswa kurejesha haraka ili pesa hizo ziweze kusaidia na wadogo zenu na kama mko hapa mchakato wake ni mfupi tu.”Amesema Badru
No comments :
Post a Comment