Monday, October 5, 2020

WIZARA YA ARDHI KUANZISHA MFUKO WA KUBORESHA MAKAZI

 


Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge akifafanua jambo
wakati akizindua Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani jijini Dodoma
leo tarehe 5 Oktoba 2020.


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze akizungumza wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyia jijini Dodoma leo
tarehe 5 Oktoba 2020.
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usanifu Miji na Mipango
Kabambe Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Immaculate Senje
akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani
yaliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.


Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge (katikati
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Idara na
Taasisi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani
yaliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kukabiliana na
changamoto za kifedha na kutekeleza matakwa ya kisera inatarajia
kuanzisha mfuko wa kuboresha makazi na ujenzi wa nyumba za gharama
nafuu.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 5 Oktoba 2020 jijini Dodoma kupitia
hotuba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
iliyosomwa kwa niaba na Mkuu wa mkoa huo Dkt Bilinith Mahenge.

Kupitia hotuba yake Waziri Lukuvi amesema, Mfuko huo una lengo la
kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata nyumba bora za gharama
nafuu au kupanga.

Amesema, Mfuko wa kuboresha Makazi utaanzishwa kwa kutumia tengeo la
bajeti ya Serikali na unatarajiwa kujiendesha kwa kutumia vyanzo
vingine vya mapato vikiwemo riba kutokana na mikopo itakayotolewa kwa
wananchi na taasisi zinazojishughulisha na maendeleo ya nyumba.

Aidha, kupitia maadhimisho hayo ya Siku ya Makazi Duniani aliziagiza
ofisi za ardhi za mikoa na mamlaka ya upangaji kusimamia kikamilifu
zoezi la utambuzi, upangaji, upimaji na umilikishaji wa makazi kwa
kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyotolewa ili kila
mwananchi mwenye kiwanja na nyumba sehemu zinazokubalika kisheria
aweze kumilikishwa.

Sambamba na hilo alizitaka Halmashauri zote nchini kuwapatia
waendelezaji miliki huduma watakazohitaji kama vile kuainisha maeneo
yaliyoiva kimipango miji, kuandaa mipango ya uendelezaji miji, kupima
viwanja na kuweka miundo mbinu.

‘’Halmashauri zinapaswa kutoa hati miliki za ardhi na vibali vya
ujenzi kwa wakati bila kusahau jukumu la msingi la kusimamia na
kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi’’ alisema Lukuvi kupitia
hotuba yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze alisema wakati
Tanzania ikiadhimisha siku ya makazi duniani inaonesha kuna uhitaji
mkubwa wa makazi bora katika maeneo ya mijini na vijini kutokana na
ongezeko la watu na kubainisha kuwa kati ya asilimia 70 hadi 80 ya
makazi nchini yapo katika maeneo yasiyo rasmi.

Amefafanua kuwa Tanzania bado ina uhaba mkubwa wa nyumba hasa kwa
wananchi wenye kipato cha chini na kubainisha kuwa zaidi ya asilimia
80 ya nyumba zilizojengwa zimegharimiwa na wananchi wenyewe.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila jumatatu ya kwanza ya mwezi
Oktoba ya kila mwaka na siku hiyo huadhimishwa kwa njia mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kutafakari hali ya makazi katika nchi na ujumbe wa
mwaka huu ni Nyumba kwa wote Miji bora ya Baadaye.

No comments :

Post a Comment