Mkurugenzi
Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma akitoa
tarifa kuhusu uzinduzi wa mpango mkakati wa Kidigitali wa Afya
unaotarajiwa kuzinduliwa Septemba 10 mwaka huu.
Mkurugenzi
wa Mafunzo wa Wizara ya Afya Mwinyi Msellem akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari kuhusu Mpango Mkakati wa wa Kijitali wa afya
Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezo 08,09,2020
WIZARA ya Afya itazindua Mpango Mkakati wa Kidigitali wa Sekta ya
Afya utakaoweka mifumo bora ya uimarisha wa huduma za Afya kwa wananchi
wa Zanzibar kuanzia mwaka huu.
Mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Afya Hamad
Rashid Muhamed tarehe 10 mwezi huu katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi
wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma amesema Mpango huo wa miaka
mitano utapunguza gharama kwa Serikali na wagonjwa.
Ameweka wazi kuwa Mpango huo utaimarisha upatikanaji wa huduma na
utarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa ambazo zitasaidia
uongozi wa Wizara kutoa maamuzi yaliyo sahihi ya afya katika wakati
muafaka.
Aidha amesema Mpango huo wa Kidigitali utaweka kumbukumbu zote muhimu
za wagonjwa watakaofika hospitali kupata huduma kwa njia ya kijitali
kutoka hospitali na vituo vyote vya afya.
Amewahakikisha wananchi kuwa Serikali imejipanga kikamilifu na
wanauhakika kuwa mpango huo utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya
afya.
Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya Mwinyi Msellem alieleza kuwa
Mpango Mkakati wa huduma za afya Zanzibar utasaidia kulinda maadili na
utaongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
Alisema baada ya kumalizika kipindi cha miaka mitano Mpango huo
utafanyiwa mapitio ili ikionekana kulikuwa na mapungufu katika
utekelezaji yaweze kufanyiwa kazi.
Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Wizara ya Afya Mohamed Habib amesema
Mpango huo pia utasaidia sekta nyengine nyengine muhimu za Serikali
ikiwemo sekta ya elimu.
Aidha alisema katika kuhakikisha Mpango huo unakuwa wa mafanikio,
wameandaa mifumo mbadala ya upatikanaji wa miundombinu ya dharura
ikiwemo huduma ya umeme na mitandao ya simu.
No comments :
Post a Comment