Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA), wakati wa uzinduzi wa vifaa stahiki vya karakana
vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, pamoja na viongozi wengine wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA), wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa
vifaa stahiki vya karakana vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Matengenezo na Huduma za Ufundi, Mhandisi Sylvester Semfukwe, akitoa
maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, wakati wa uzinduzi wa vifaa
stahiki vya karakana vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA),
wakati akikagua baadhi ya vifaa stahiki vilivyonunuliwa kwa ajili ya
karakana za Wakala huo katika mikoa yote nchini.
Baadhi ya vifaa stahiki
vilivyonunuliwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa ajili ya
kuboresha na kuziongezea ufanisi katika utendaji kazi wa karakana na
vitasambazwa katika mikoa yote nchini. Vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya
shilingi milioni 430.
…………………………………………………………………………………..
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano imekabidhi kwa Wakala wa Ufundi na umeme (TEMESA) vifaa
stahiki kwa ajili ya karakana za mikoa 14 na kituo kimoja (1) kikubwa
vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 430 kwa lengo la kuboresha
huduma za utengenezaji wa magari.
Vifaa hivyo vitagawiwa katika
katika mikoa/vituo vya wakala huo vilivyopo Dar es Salaam (Vingunguti),
Mtwara, Mara, Simiyu, Kagera, Tabora, Iringa, Rukwa, Manyara, Arusha,
Kilimanjaro, Tanga, Songwe na Same.
Aidha, imeelezwa kuwa hii ni
muendelezo wa awamu ya kwanza ya vitendea kazi vilivyosambazwa kwenye
karakana za mikoa 12 na vituo viwili (2) vikubwa katika mwaka wa fedha
2019/2020 na kuleta tija katika utoaji huduma bora kwa wateja na
kuongeza mapato.
Akizunguma wakati wa uzinduzi
huo wa vifaa hivyo uliofanyika katika karakana ya MT. DEPOT jijini Dar
es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius
Mwakalinga, ameupongeza wakala huo kwa kuanza ukurasa mpya katika mikoa
yote nchini ili kuondoa zile kero na malalamiko ya matengenezo ya magari
yaliyokuwa yanatolewa dhidi yao.
“Kupokea vifaa ni jambo moja
na kuvitumia, kuvitunza ni jambo lingine hivyo tumieni vifaa hivi kuleta
tija na kuongeza ufanisi zaidi”, amesema Arch. Mwakalinga.
Mwakalinga, ameongeza kuwa
Wizara ipo kwa ajili ya kuendelea kuiwezesha wakala kutekeleza majukumu
yake ya msingi kwa ufanisi na kasi zaidi ili kupunguza malalamiko ya
wateja hususan katika matengenezo ya magari.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni
rasmi, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Masele, amesema kuwa
Wakala umeendelea kuzifanyia ukarabati karakana zake katika mikoa ya Dar
es Salaam (Vingunguti), MT Depot, Dodoma, Singida, Mwanza na Mbeya
katika mwaka wa fedha 2019/2020 na katika mwaka huu mpya wa fedha
2020/21 imeweka mpango wa ukarabati katika karakana za mikoa ya Mara,
Tabora, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Kigoma, Arusha na Pwani.
Katika kuhakikisha huduma
zinasogezwa karibu na mteja, Mhandisi Masele ameeleza kuwa Wakala
umepanga kuanzisha karakana kwenye Wilaya zilizo umbali wa kilometa 120
kutoka katika karakana ya mkoa.
“Wakala tayari umeshaanzisha
karakana za Wilaya katika Wilaya za Kilombero na Kahama ambazo
zinaendelea kutoa huduma na sasa tuko mbioni kuanza huduma katika
karakana ngazi ya Wilaya katika mji wa Same Mkoani Kilimanjaro”,
amefafanua Mhandisi Masele.
Mtendaji Mkuu Masele
amemueleza pia Katibu Mkuu Mwakalinga kuwa Wakala unaendelea kukamilisha
ukarabati wa miundombinu na majengo kwa ajili ya karakana ya Mkoa wa
Songwe itakayoanza kazi rasmi mapema mwezi Septemba 2020.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Bodi ya ya Ushauri ya Wakala huo TEMESA, Prof. Idrissa Mshoro,
ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini TEMESA na kutoa fedha za
kununua vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya karakana zote nchini na
kuahidi na kuendelea kutoa ushauri stahiki katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazoukabili wakala huo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment