Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi
akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wiki moja ya mbinu za utafiti
kwa wataalamu wa kada mbalimbali yaliyofanyika hospitalini hapa.
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo
hayo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi SAhirikishi Muhimbili-MUHAS,
Prof. Method Kazaura akiwasilisha mada.
Wataalamu wakifuatilia kwa makini mada katika mafunzo hayo.
Dkt. Magandi katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
…………………………………………………………..
Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila imefungua mafunzo ya wiki moja kwa washiriki 25 wa
kada mbalimbali yanayolenga kuwapa ujuzi wa mbinu za utafiti ili
kuboresha utoaji huduma za afya kwa watanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba
ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa
uongozi wa
hospitali ya Muhimbili Upanga na Mloganzila unaunga mkono mafunzo ya
wataalamu mahali pa kazi kwani yatasaidia kuboresha utoaji huduma.
“Napenda kusisitiza kuwa bodi ya
wadhamini na uongozi wa MNH tunaunga mkono ufanyaji wa tafiti hizi kwa
maslahi mapana ya taifa letu na maboresho ya utoaji huduma za afya
katika hospitali yetu.” Amesema Dkt. Magandi.
Sambamba na hilo Dkt. Magandi
ameeleza kuwa ili kuweza kufikia mapinduzi makubwa katika sekta ya afya
hatuna budi kujikita katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali kama ilivyo
katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani, Uingereza, China na Afrika
ya Kusini ambazo ni baadhi tu ya nchi zinazofanya tafiti nyingi na
kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya.
Aidha Dkt. Magandi ametaja moja ya
faida za utafiti kuwa ni pamoja na kuwasaidia watafiti na wataalamu wa
afya katika kada zote kupata njia mpya na sahihi za kuelewa, kugundua,
kudhibiti na kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu.
Mafunzo
hayo yataendeshwa na wataalamu bobezi katika tafiti za afya kutoka Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili- MUHAS kwa kusimamiwa na
Kitengo cha Elimu, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu MNH-Mloganzila.
No comments :
Post a Comment