Tuesday, September 8, 2020

KONGWA INA FURSA YA KULIMA KOROSHO NA MKONGE-KUSAYA



Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo  Bw.Gerald Kusaya akikagua mti bora wa mkorosho weye umri wa miaka miwili katika shamba la mkulima Berling Sospeter wa kijiji cha Makutani wilaya ya Kongwa jana alipotembelea kuhamasisha kilimo cha korosho.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (laiyevaa koti la blu) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt.Suleiman Serera (aliyevaa miwani) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa Dkt.Omary Nkullo (wa kwanza kushoto) alipokagua shamba la korosho kijiji cha Makutani jana.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa akitazama mti bora wa mkorosho jana alipotembelea shamba la mkulima kijiji cha Makutani wilaya ya Kongwa kuhamasisha kilimo cha mazao ya biashara ikiwemo zao la mkonge linalostawi vema.Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe.Dkt.Suleiman Serera na kulia Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Omary Nkullo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiendesha moja kati ya pipikipi tatu zenye thamani ya shilingi milioni 15 alizokabidhi jana kwa maafisa ugani kilimo wa wilaya ya Kongwa ili zitumike kuhamasisha kilimo cha mazao ya korosho na mkonge.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (katikati) akiwa na viongozi wa wilaya ya Kongwa mkoa wa Dodoma jana alipotembelea kijiji cha Makutani kuhamasisha kilimo cha mazao ya korosho na mkonge yanayostawi vema.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt.Suleiman Serera.
Makabidhiano ya pikipiki kwa ajili ya kuwezesha maafisa ugani kilimo kuwahudumia wakulima.Pichani Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa akionyesha fungua tatu za pikipiki alizozitoa kwa Halmashauri ya Kongwa na kupokelewa na Mkurugenzi wake Dkt.Omary Nkullo (katikati) Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Suleiman Serera akishuhudia makabidhiano hayo jana kijiji cha Mbande.
(Habari na Picha na Wizara ya Kilimo)
…………………………………………………………………..
Wakulima wa wilaya ya Kongwa mkoa wa Dodoma wamehamasishwa kuanzisha mashamba ya
korosho na mkonge yanayostawi na kuvumilia hali ya ukame ili wawe na mazao ya biashara ya kudumu yatakayowapatia kipato cha uhakika.
Wito huo umetolewa jana (07.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipotembelea kijiji cha Makutani wilayani Kongwa kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la korosho walilioanza kulima mwaka 2018.
Kusaya alifahamishwa na viongozi wa wilaya hiyo kuwa katika msimu wa mwaka 2019/20 miche 303,095 ya korosho bora iligawiwa na kupandwa na wakulima wapatao 386 wa wilaya hiyo na kuwa mwaka huu 2020/21 jumla ya kilo 3,000 (tani 3) za mbegu bora ya korosho imeagizwa toka kituo cha utafiti (TARI) Naliendele ili igawiwe kwa wakulima, vikundi na taasisi  .
“ Pamoja na korosho wakulima wa Kongwa limeni mkonge kwa kuwa unavumilia hali ya hewa ya ukame .Ukipanda leo mkonge baada ya miaka mitatu utaanza kuvuna na kuendelea hadi baada ya miaka kumi na tano” alisisitiza Kusaya
Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo aliongeza kuwa wakulima wakihamasishwa wataweza kupanda mkonge kwa kuwa sasa unalimwa vizuri kwenye mikoa 17 ya Tanzania bara ikiwemo Dodoma.
Ili kufikia ufanisi na kuongeza uzalishaji wa mazao ya korosho na mkonge, Kusaya alisema wizara ipo tayari kupeleka wataalam wa mazao hayo wilayani Kongwa kuwafundisha mafisa ugani Kilimo bora na chenye kulenga kuongeza uzalishaji ili wawasaidie wakulima vijijini.
Awali Kusaya alitembelea shamba la korosho la mkulima Berling Sospeter wa kijiji cha Makutani lenye ukubwa wa ekari 325 na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya .
Mkulima alitataji changamoto ya upatikanji wa madawa ya kupulizia mikorosho na tatizo la mifugo kuwa linathiri shamba lake hivyo, kuiomba Wizara ichukue hatua kudhibiti uwepo wa madawa yasiyo na ubora.
Katika kutekeleza adhma hiyo Katibu Mkuu Kusaya alikabidhi pikipiki tatu zenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt.Omary Nkullo ili ziwasaidie maafisa ugani kuwafikia wakulima vijijini
“Leo nimekukabidhi DED pikipiki hizi tatu ili ziweze kutumika na maafisa ugani kusimamia uanzishwaji mashamba ya korosho na mkonge .Nataka maafisa Kilimo wasikae ofisini waweze kwenda vijijini kuhudumia wakulima kuongeza uzalishaji” alisema Kusaya.
Akizungumza kwenye ziara hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Omary Nkullo alisema wamepanga kuzalisha miche bora ya korosho 420,000 ili igawiwe kwenye kata zote 22 ili wakulima wengi walime zao hilo la biashara .
Dkt. Nkullo aliomba wizara ya kilimo kuwezesha na kusimamaia wataalam wa kilimo kupata mafunzo ya kina ili wawe na ujuzi wa kufundisha wakulima kilimo cha korosho na mkonge pia kuwapatia vitendea kazi .
“Halmashauri ya Kongwa kuna maafisa ugani 58 lakini wote hawana usafiri wa kuwaaidia kuwatembelea wakulima,tunaomba wizara itusaidie pikipiki Zaidi ya hizi tatu ili zitumike kuhamasisha Kilimo “ aliomba DED Kongwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa aliyeshiriki katika ziara hiyo Dkt.Suleiman Serera alisema tangu ameteuliwa kuongoza wilaya hiyo amekuwa akifanya ziara vijijini ambapo amegundua utayari wa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara ikiwemo korosho, mkonge na karanga lakini wanakosa wataalam wa kuwafundisha kwa karibu.
Dkt.Serera aliongeza kusema wanahitajika maafisa ugani wengi zaidi ili kuwezesha lengo la serikali kuongeza uzalishaji mazao ya biashara ya korosho na mkonge ili wakulima wafahamu kanuni bora za uzalishaji na kuwa na tija.
Alitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kwenda Kongwa kwani kuna ardhi nzuri ya kutosha hususan kuanzisha mashamba ya umwagiliaji kutokana na uwepo wa zaidi ya hekta 5,000 zinazofaa.
“Tunalo eneo la hekta 5,811 zinazofaa kwa umwagiliaji ambapo kwa sasa ni hekta 372 pekee zinatumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Natoa rai kwa wawekezaji kuja Kongwa kuanzisha mashamba makubwa ya umwagiliaji” alisisitiza Dkt.Serea
Kwa mujibu wa taarifa ya wilaya ya Kongwa ilionesha kuwa katika msimu wa kilimo mwa 2019/20 ilizalisha tani 302,738 za chakula cha wanga ukilinganisha na mahitaji ya tani 87,476 hivyo kuwa na ziada ya tani 215,261 za chakula cha wanga kutokana na uwepo wa mvua za kutosha.
Aidha katika kipindi hicho cha 2019/20 wilaya ya Kongwa ilizalisha tani 80,579 za mazao ya biashara na mazao jamii ya mikunde/protini wilaya imezalisha tani 6,025 hali inayowafanya wakulima wawe na uhakika wa kipato .

No comments :

Post a Comment