**************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
TMA imesema mvua za Vuli zinatarajia kuwa za chini ya wastani hadi
wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo
mengi ya nchi.
Ameyasema hayo leo Mkurugenzi Mkuu
TMA,Dkt. Agnes Kijazi kwenye mkutano na
waandishi wa habari
uliofanyika Makao Makuu ya TMA jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano huo
Dkt.Kijazi amesema Mvua za Vuli zinatarajia kuanza kwa kuchelewa kati ya
wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba mwaka huu katika maeneo ya
nyanda za juu Kaskazini Mashariki na ukanda wa Pwani ya Kaskazini pamoja
na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.
Aidha Dkt.Kijazi amesema Mamlaka
ya Hali ya Hewa inatoa ushauri kwa kushirikiana na wadau katika sekta
husika ili kukabiliana na athari mbalimbali zinazotarajiwa kujitokeza.
“Tunatarajia kwamba kutakuwa na
Upungufu wa unyevunyevu katika udongo hivyo sekta husika inaweza
kuangalia ni namna gani wanaweza kujiandaa vizuri kwaajili ya
kukabiliana na visumbufu vya mazao na magonjwa mbalimbali ambayo
yanajitokeza na ambayo yanatarajiwa kuongezeka.
Hata hivyo amesema wakulima
wanashauriwa kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa ndani ya muda
mfupi pia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi
unyevunyevu na maji zinashauriwa kutumika.
Pamoja na hayo Dkt.Kijazi amesema
kutokana na utabiri huo sekta ya usafirishaji inatarajiwa kunufaika
hususani katika usafiri wa anga na nchi kavu.
“Sekta husika wanashauriwa kutumia
muda huu kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji hasa kwa
ujenzi unaohusisha maeneo yanayoathiriwa na mafuriko”. Amesema
Dkt.Kijazi.
No comments :
Post a Comment