Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Nchimbi akifungua mkutano mkuu
wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara,
uliofanyika mjini Babati jana, kushoto ni Mwenyekiti wa Mviwata Mohamed
Hussein na Mratibu wa Mviwata Martin Pius.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Nchimbi (kushoto) akikagua
mazao ya wakulima kwenye mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya
wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati.
Wadau wa kilimo
wakiwa katika picha ya pamoja kwenye mkutano mkuu wa 13 wa Mtandao wa
vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika mjini Babati

Mwenyekiti wa Mviwata
Manyara, Mohamed Hussein akisoma taarifa kwenye mkutano mkuu wa 13 wa
Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) Mkoa wa Manyara, uliofanyika
mjini Babati.
………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Babati
WAKULIMA wametakiwa
kugomea vipimo visivyo rasmi vya magunia na madebe wakati wa kupima
mazao yao kwani vinawanyonya hivyo watumie mizani ili kuepuka
kudhulumiwa haki zao.
Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya ya Babati, John Nchimbi aliyasema hayo kwenye
mkutano wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) mkoani
Manyara.
Nchimbi alisema
wakulima wanapaswa kutambua kuwa vipimo vya ubabaishaji na wizi vya
magunia na madebe hayapaswi kutumika kwa sasa kwa hiyo wagomee hilo na
kusisitiza kuwepo kwa vipimo kwa kilo.
Alisema serikali
itawaunga mkono kwenye hilo endapo wao wenyewe watakuwa na msimamizi
mkali wa kuepuka kunyonywa mazao yao ili wakulima wapate tija na kuepuka
kudhulumiwa.
“Mviwata haiwezi kukulinda wala serikali haitaweza kukusaidia endapo mkulima mwenyewe hautagomea vipimo vya wizi na ubabaishaji dhidi ya mazao ya mkulima.
Hata hivyo, alisema
baadhi ya wakulima wanaweza kuwa vikwazo kwa wenzao kwa kukubali kutumia
vipimo vya magunia na madebe kutokana na tamaa ya muda mfupi badala ya
kuwa na msimamo.
Mratibu wa Mviwata
mkoani Manyara, Martin Pius alisema wamekuwa karibu na wakala wa vipimo
Tanzania juu ya kutumika kwa mizani huku wakitoa elimu na mbinu
mbalimbali za kubaini vipimo halisi.
Pius alisema kupitia
mitandao yao mkoani Manyara wamekuwa wakiwaelimisha wakulima namna ya
kutumia mizani kwenye upimaji wa mazao na kuachana na mtindo wa kutumia
magunia na madebe.
“Pia wakulima
wameendelea kujifunza mbinu mbalimbali za kutambua mizani zinazowaibia
wakulima kwa lengo la kuhakikisha wananufaika na mazao yao pindi
wakipima uzito wa mazao yao,” alisema Pius.
Alisema walizungumza
na wakala wa vipimo nchini ili kuziwezesha halmashauri kutunga na
kupitisha sheria ndogo za kutumia mizani za kupima mazao hasa vijijini.
Mmoja kati ya
wakulima wa kijiji cha Galapo, Hamis Ibrahim aliipongeza Mviwata kwa
namna wanavyoingilia kati suala zima la matumizi ya vipimo kwa wakulima
wa eneo hilo.
Alisema awali ilikuwa
vigumu wakulima kutekeleza hilo ila Mviwata walizunguka kwa wakulima
mbalimbali na kutoa elimu hadi wakatambua haki zao.
No comments :
Post a Comment