Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa
wa Rukwa Benjamin Mangwala akitoa nasaha kwa viongozi wa vyama vya
ushirika katika kuhakikisha wanazingatia sheria za kuingia mikataba ya
mikopo na kampuni za usamabazaji dhana bora za kilimo.
Kaimu Meneja wa Kampuni ya Agricom
Africa Remy Lindi akielezea zana za kilimo zinazosambazwa na kampuni
hiyo katika mkoa wa Rukwa ili kuwapa fursa wakulima wa mkoa huo kulima
kwa tija.
Afisa zana za kilimo mkoa wa Rukwa
Mhandisi Sebastian Kioyo akielezea faida za matumizi ya zana bora za
kilimo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika (hawapo pichani)
katika uzinduzi wa Programu ya matumizi Bora ya Zana za kilimo mkoa wa
Rukwa.
kaimu Katibu Tawala Msaidizi
Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Rukwa Ocran Chengula akijaribu
moja ya zana za kilimo zinazosamabazwa na kampuni ya Agricom kujionea
ubora wa zana hizo mara tu baada ya mafunzo ya zana hizo.
…………………………………………………………………
Vyama vya
Ushirika Mkoani Rukwa vimetakiwa kuwekeza nguvu zao katika upatikanaji
wa
zana bora za kilimo ili kuweza kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao
mbalimbali mkoani Rukwa hasa katika kipindi hiki wanachojiandaa kuanza
msimu mpya wa kilimo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.
Akiongea wakati
wa Ufunguzi wa uzinduzi wa Mkakati wa matumizi bora ya zana za kilimo,
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa
Rukwa, Ocran Chengula alisema kuwa, asilimia 80 ya uchumi wa Mkoa wa
Rukwa unategemea kilimo lakini ni asilimia 3 tu ya wakulima wanatumia
matrekta hali inayopekelea eneo kubwa la ardhi inayofaa kulimwa katika
mkoa huo kutolimwa na pia kutopata mazao bora yenye kuhimili ushindani
katika soko la dunia.
“Katika mkoa wetu
kuna hekta 1,660,000 ambazo zinafaa kwa kilimo, lakini kati ya hizo kwa
kiasi kikubwa sana tunazoloma ni hekta laki tano na kidogo, ambazo ni
sawa na asilimia 32 kuna kipindi tulifika hadi asilimia 35 lakini ni
kiasi kidogo sana, na kitu ambacho kinatukwamisha katika kuongeza eneo
la kilimo ni kutumia zana ambazo sio Rafiki kwa kilimo, katika mkoa wetu
kwa kiasi kikubwa sana (75%) tunatumia zana za kukokotwa na ng’ombe kwa
maana ya maksai,” Alisema.
Wakati akielezea
mpango wa serikali kuhakikisha wanavitumia vyama vya ushirika ili
kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kulima kwa tija, Mrajisi wa Vyama vya
Ushirika mkoani Rukwa Benjamin Mangwala alisema kuwa, Tume ya Maendeleo
ya Ushirika nchini imeridhia vyama hivyo kuingia mikataba ya mauziano
na matumizi ya zana bora za kilimo na makampuni ya usambazaji wa zana
hizo ili kuondokana na matumizi ya zana duni huku akifafanua sheria
zitakazolinda mikataba hiyo.
“Hiyo sheria ya
Ushirika ya mwaka 2013 inaekeleza kwamba maamuzi ya kuweza kununua hayo
matreka yatatokana na maamuzi ya wanachama husika na si vinginevyo kwa
maana nyingine ni kwamba pale ambapo azimio litafanyika wakati
mahudhurio ya wanachama yapo chini kwa mujibu wa sheria, azimio hilo
halitakuwa halali na hivyo chama husika kitaathirika kwa kushindwa
kukidhi sifa za hilo azimio, hata kama walikuwa na sifa ya kupata hicho
kifaa, hivyo niwaombe viongozi wa vyama vya ushirika na maafisa ushirika
mshirikiane,” Alieleza.
Kwa upande wake
Kaimu Meneja wa kampuni ya Agricom African Limited Remy Lindi alisema
kuwa wameamua kufika mkoani Rukwa baada ya kuona wakulima wengi
wanashindwa kulima kwa tija kutofikia malengo kwasababu ya kukosa zana
bora za kilimo ambazo kampuni hiyo inaagiza na kuzisambaza kwa wakulima.
“Agricom tumeamua
kuja huku na kutoa hii elimu ya utumiaji wa zana hizi bora ili mwisho
wa siku waweze kuhama na kubadilika na kuona manufaa kwasababu huwezi
kumshawishi mtu kutumia zana pasipokuelewa faida yake, ndio maana
tunasema shamba pesa maana yake ni kwamba lazima ufanye vitu kitaalamu
na kisasa ili kuweza kupata pesa kutoka shambani,” Alimalizia.
Miongoni mwa
wafaidika wa elimu hiyo ya matumizi bora ya zana za kilimo Mwenyekiti wa
Kanyele AMCOS Esther Sikozi alisema kuwa, ujio wa vifaa hivyo
utawapunguzia kazi kwani ukilimakwa kutumia Wanyama kazi unatumia siku
mbili hati tatu kumaliza ekari moja wakati trekta linatumia dakika
chache kulima ekari moja.
Mkoa wa Rukwa una
vyama vya ushirika 166 huku 88 vikiwa vinajihusisha na kilimo na ni
vyama 29 pekee ndivyo vyenye sifa za kukopesheka na hiyo ni baada ya
kuvuka kigezo cha kuwa na idadi kadhaa ya wanachama ambao wanaweza
kuchangia ili kuweza kulipa mkopo wa trekta la kulimia.
Maelezo ya Picha
DSC_0458 – Baadhi
ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa wakipata mafunzo ya
matumizi ya dhana bora za kilimo wakati wakijiandaa na msimu mpya wa
kilimo.
No comments :
Post a Comment