
………………………………………………………………………
Na. Edward Kondela
Watanzania
wametakiwa kunywa maziwa kwa kuwa ni chakula bora kwa afya ya binadamu
na kwamba hitaji la soko la maziwa kadri linavyoongezeka serikali
itaweza kufikia azma ya
falsafa ya uchumi unaotegemea viwanda.
Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema hayo mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro akiwa katika
mazungumzo na Katibu Tawala wa mkoa huo Dkt. Khatibu Kazungu pamoja na
baadhi ya viongozi wa mkoa na mwakilishi kutoka Bodi ya Maziwa nchini
(TDB), kuhusu programu ya mradi wa kitaifa wa unywaji maziwa shuleni
utakaoadhamishwa kitaifa tarehe 30 Septemba 2020 Mkoani Kilimanjaro.
Prof. Gabriel
amesema mradi huo ambao umeingia nchini mwaka 2007 ukijumuisha nchi
sabini hadi sasa kwa utaratibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO),
umelenga kusaidia kuwapatia watoto afya nzuri wakiwa masomoni, kuwafanya
watoto kupenda shule na kujenga hamasa kwa watoto wakiwa wakubwa waweze
kushiriki na kujua umuhimu wa kunywa maziwa.
“Wito ni
kwamba programu hii inasaidia sana kuwajengea watoto afya nzuri, lakini
pia kusaidia watoto wapende kwenda shuleni kwa maana ya uwepo wa maziwa
shuleni ni kivutio kimojawapo, lakini pia kujenga hamasa vijana wetu
wanapokuwa wakubwa waweze kushiriki na kutambua umuhimu wa kunywa maziwa
katika mhimili mzima wa afya zetu.” Amesema Prof. Gabriel.
Aidha, Prof.
Gabriel amefafanua kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita Bilioni
3.04 kwa mwaka, hivyo miradi ya namna hii ina umuhimu wake hasa kwa
ajili ya mipango endeleveu ya maziwa pamoja na uwepo wa ongezeko la
viwanda vya kuchakata maziwa nchini na kufikia falsafa ya serikali ya
kufikia uchumi unaotokana na viwanda.
Kwa upande wake
Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Khatibu Kazungu amesema mkoa huo
umepata faraja kupewa nafasi ya kuandaa tukio hilo kubwa la kidunia kwa
mara ya pili na kwamba mkuu wa mkoa huo anatarajia kuwa mgeni rasmi
wakati wa maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa
suala la unywaji wa maziwa ni muhimu kwa ajili ya afya ya binadamu na
kwamba watoto wengi wamekuwa wakienda shuleni wakiwa hawajapata chakula
asubuhi, hivyo uwepo wa maziwa shuleni kutawafanya watoto waweze
kuchangamsha akili zao.
Programu ya mradi wa kitaifa wa unywaji wa maziwa shuleni, mwaka huu umebeba kauli mbiu “Glasi Moja ya Maziwa kila siku kwa Afya na Elimu Bora”.
Maadhimisho hayo yamebeba
madhumuni ya kuwa na siku moja ambayo fikra za watu wote zitaelekezwa
kwenye manufaa ya mpango wa maziwa shuleni na hivyo kuhamasisha
kuanzishwa kwa mpango huo.
No comments :
Post a Comment