Wahandishi
wa umwagiliaji wa mikoa wameagizwa kujipanga kwa kasi kusimamia na
kutekeleza agizo la Serikali ya Awamu ya Tano la kuhakikisha eneo la
kilimo cha umwagiliaji linaongezeka toka hekta 694,715 hadi kufikia
hekta milioni moja ifikapo mwaka 2025.
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ametoa agizo hilo jana (16.09.2020)
alipofungua kikao kazi cha Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
na Wahandisi wa umwagiliaji toka mikoa ya Tanzania Bara kilichofanyika
mkoani Morogoro.
Kusaya
amesema ni wakati muafaka kwa wahandisi wote wa umwagiliaji nchini
kujikita katika kuweka mipango inayotekelezeka ili eneo la umwagiliaji
linalolimwa sasa liongezeke na tija ipatikani kwa wakulima.
“Malengo
ya Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Umwagiliaji ni kuhakikisha
kuwa hekta 1,000,000 zinafikiwa katika kilimo cha umwagiliaji ifikapo
mwaka 2025 hivyo leo hii mtaniambia je kasi tunayokwenda nayo inatosha?”
alisema Kusaya
Katika
hotuba yake ya ufunguzi Katibu Mkuu alibainisha kuwa Wizara ya kilimo
inataka Tume ya Umwagiliaji kujikita zaidi katika kutatua changamoto za
miundombinu ili wakulima wazalishe mazao kwa wingi kuwezesha nchi kuwa
na uhakika wa chakula.
Aliipongeza
tume ya umwagiliaji kwa mafanikio ya kuongeza eneo ambapo katika
kipindi cha mwaka 2015 hadi Septemba, 2020 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
imefanikiwa kujenga na kukarabati jumla ya skimu 179 za Umwagiliaji na
hivyo kufanikiwa kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000
mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020.
Katibu
Mkuu huyo aliongeza kusema tija ya uzalishaji imeongezeka katika skimu
za umwagiliaji kutoka wastani wa tani 1.8 – 2.0 kwa hekta hadi kufikia
wastani wa tani 4.0 – 5.0 kwa hekta kwa zao la mpunga na zao la mahindi
uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1.5 hadi tani 3.7- 5.0 kwa hekta.
“Lengo
tunataka kilimo cha umwagiliaji kiwe endelevu na kumsaidia mkulima kuwa
na kipato kikubwa kutokana na uwepo wa ardhi nzuri na mabonde yanayofaa
kwa umwagiliaji na nchi kuwa na uhakika wa chakula ” alisisitiza
Kusaya.
Kusaya
aliwagiza pia wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa na watumishi wote
kuwa na utumishi wenye tija zaidi na matokeo makubwa, kufanya kazi kwa
kuzingatia uzalendo, weledi, kujituma kwa bidii, kuwa wabunifu,
kushirikiana kama timu moja katika kutekeleza majukumu ya Tume huku
wakizingatia maadili ya utumishi wa Umma ambayo ndiyo Dira katika
kuufikia Utumishi uliotukuka na kuitendea haki Kauli Mbiu ya Mhe Rais ya
“HAPA KAZI TU”.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
Eng.David Kaali alisema wamefanikiwa kuongeza uzalishai wa mpunga
kupitia skimu za umwagiliaji kutoka tani 714,000 mwaka 2000 hadi kufikia
tani 2,009,174 mwaka 2019 kutokana na miundombinu mingi kuboreshwa.
Aidha,
aliongeza kusema tume imefanikiwa pia kujenga na kukarabati skimu 179
za umwagiliaji nchini na kuongeza uwezo wa mitambo kufikia 56 inayofanya
kazi kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika mikoa yote.
Ili
kufikia lengo la hekta milioni moja ifikapo mwaka 2025 Tume itaendeleza
mabonde ya umwagiliaji yafuatayo bonde la mto Ruvuma hekta (
26,000),mto Ruhuhu (3,700),mto Songwe (3,005), mto Rufiji (64,896),
bonde la Luiche Kigoma (3,000) na bonde la Usangu- Mbeya ( 10,000)
katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2021-2025.
Mhandisi
Kaali alisema ili mkakati huo wa kuongeza eneo la umwagiliaji ufanikiwe
Tume itahitaji kiasi cha Shilingi Bilioni 986.8 ambapo serikali
itachangia asilimia 41 na kiasi kingine kitatokana na vyama vya
umwagiliaji,wadau na sekta binasfi kama ilivyoanishwa katika Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
Katika
hatua nyingine Mhandisi Kaali ameiomba serikali kutoa kipaumbele kwa
Tume kuweza kupata wataalam ili kupunguza tatizo ambapo mahitaji ni 646
waliopo ni 208 na kuwa na upungufu wa wataalam 438 kote nchini.
No comments :
Post a Comment