Watanzania
wametakiwa kunywa maziwa kwa kuwa ni chakula bora kwa afya ya binadamu
na kwamba hitaji la soko la maziwa kadri linavyoongezeka serikali
itaweza kufikia azma ya falsafa ya uchumi unaotegemea viwanda.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel amesema hayo mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro akiwa katika
mazungumzo na Katibu Tawala wa mkoa huo Dkt. Khatibu Kazungu pamoja na
baadhi ya viongozi wa mkoa na mwakilishi kutoka Bodi ya Maziwa nchini
(TDB), kuhusu programu ya mradi wa kitaifa wa unywaji maziwa shuleni
utakaoadhamishwa kitaifa tarehe 30 Septemba 2020 Mkoani Kilimanjaro.
Prof.
Gabriel amesema mradi huo ambao umeingia nchini mwaka 2007 ukijumuisha
nchi sabini hadi sasa kwa utaratibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO),
umelenga kusaidia kuwapatia watoto afya nzuri wakiwa masomoni,
kuwafanya watoto kupenda shule na kujenga hamasa kwa watoto wakiwa
wakubwa waweze kushiriki na kujua umuhimu wa kunywa maziwa.
“Wito
ni kwamba programu hii inasaidia sana kuwajengea watoto afya nzuri,
lakini pia kusaidia watoto wapende kwenda shuleni kwa maana ya uwepo wa
maziwa shuleni ni kivutio kimojawapo, lakini pia kujenga hamasa vijana
wetu wanapokuwa wakubwa waweze kushiriki na kutambua umuhimu wa kunywa
maziwa katika mhimili mzima wa afya zetu.” Amesema Prof. Gabriel.
Aidha,
Prof. Gabriel amefafanua kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita
Bilioni 3.04 kwa mwaka, hivyo miradi ya namna hii ina umuhimu wake hasa
kwa ajili ya mipango endeleveu ya maziwa pamoja na uwepo wa ongezeko la
viwanda vya kuchakata maziwa nchini na kufikia falsafa ya serikali ya
kufikia uchumi unaotokana na viwanda.
Kwa
upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Khatibu Kazungu
amesema mkoa huo umepata faraja kupewa nafasi ya kuandaa tukio hilo
kubwa la kidunia kwa mara ya pili na kwamba mkuu wa mkoa huo anatarajia
kuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo.
Ameongeza
kuwa suala la unywaji wa maziwa ni muhimu kwa ajili ya afya ya binadamu
na kwamba watoto wengi wamekuwa wakienda shuleni wakiwa hawajapata
chakula asubuhi, hivyo uwepo wa maziwa shuleni kutawafanya watoto waweze
kuchangamsha akili zao.
Programu
ya mradi wa kitaifa wa unywaji wa maziwa shuleni, mwaka huu umebeba
kauli mbiu “Glasi Moja ya Maziwa kila siku kwa Afya na Elimu Bora”.
Maadhimisho
hayo yamebeba madhumuni ya kuwa na siku moja ambayo fikra za watu wote
zitaelekezwa kwenye manufaa ya mpango wa maziwa shuleni na hivyo
kuhamasisha kuanzishwa kwa mpango huo.
No comments :
Post a Comment