Balozi
wa Uingereza nchini Tanzania Bw. David Concar, akizungumza na wanufaika
wa Programu ya Mafunzo ya Uzamili katika Vyuo mbalimbali nchini
Uingereza kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kwa ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (UKaid), katika hafla ya kuwaaga,
jijini Dar es Salaam.
Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila,
(kulia) akizungumza jambo na Mkuu wa Programu ya Mafunzo wa British
Council Tanzania, Bi. Atiya Sumar, baada ya hafla ya kuwaaga Watumishi
watano wa Wizara ya Fedha na Mipango wanaokwenda kusoma Uingereza kwa
ufadhili wa UKaid.
Balozi
wa Uingereza nchini Tanzania Bw. David Concar (wa tatu kulia) na Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, (wa nne
kushoto), wakiwa katika mazungumzo na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Maafisa wa Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania na British
Council Tanzania, kabla ya hafla ya kuwaaga watumishi wa Wizara hiyo
wanaokwenda kwenye mafunzo katika vyuo mbalimbali vya Uingereza.
Wanufaika wa
Programu ya Mafunzo ya Uzamili katika Vyuo mbalimbali nchini Uingereza
kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo
la Kimataifa la Uingereza (UKaid), pamoja na wageni waalikwa wakiwa
katika hafla ya kuwaaga watumishi hao, jijini Dar es Salaam.
Wanufaika
wa Programu ya Mafunzo katika Vyuo mbalimbali vya Uingereza kwa
ufadhili wa UKaid awamu ya nne, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango,
kutoka kushoto ni Bw. Innocent Lema, Edwin Nalaila, Bi. Paulina
Fungameza, William Mhehe na Alpha Temu wakiwa katika picha ya pamoja.
(Picha na Ivona Tumsime, WFM, Dar es Salaam)
****************************************
Na Ivona Tumsime na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Watumishi wa
Wizara ya Fedha na Mipango, waliopatiwa ufadhili wa masomo katika vyuo
mbalimbali nchini Uingereza kwa mwaka 2020/2021 wametakiwa kutumia fursa
watakazozikuta kuongeza ujuzi ili kulisaidia taifa watakapomaliza
mafunzo yao.
Hayo
yameelezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bw. Doto James wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi
waliopata ufadhili wa masomo katika vyuo mbalimbali kupitia Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (UKaid).
Dkt.
Kayandabila alisema kuwa udhamini wa masomo unaotolewa na UKaid umekuwa
na faida kubwa kwa nchi kwa kuwa wale waliomaliza mafunzo kwa awamu
zilizopita kuaanzia mwaka 2017 wamekuwa na tija na ufanisi katika
kutekeleza majukumu yao ya kila siku na ndio sababu wamepangiwa majukumu
mengine mbalimbali.
“Kutokana na
umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi tunaiomba Uingereza kusaidia
pia kutoa Kozi za muda mfupi zinazohusiana na Uchumi na Utawala wa
Fedha, zitakazoongeza uwezo wa Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango
kuwa na umahiri katika utendaji wa majukumu yao”, alisema Dkt.
Kayandabila.
Aidha Dkt.
Kayandabila ameipongeza Uingereza kwa jitihada zake za kuisaidia
Tanzania katika kuongeza ujuzi, maarifa na ubunifu kwa watumishi jambo
ambalo limeongeza uimara wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali za
maendeleo hasa za kiuchumi.
Kwa upande
wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar, alisema kuwa
nchini Uingereza kuna fursa nyingi hivyo ni vema watumishi wakazitumia
vizuri ili kuongeza ujuzi na ufanisi kwa kusoma kwa bidii na
watakaporudi waweze kuisaidia Wizara na wananchi katika masuala
mbalimbali yakiwemo ya uchumi, sheria na Sayansi ya Kompyuta.
“Watumishi wa
Wizara ya Fedha na Mipango watakaporudi nchini na kuweza kulisaidia
Taifa itakuwa ni chachu ya watanzania wengine kuhamasika kwenda kupata
ujuzi na maarifa nchini Uingereza”, alieleza Balozi Concar.
Naye Mkuu wa
Programu za Mafunzo wa British Council, Bi. Atiya Sumar, alisema kuwa
uwepo wa British Council nchini Tanzania miaka 17 iliyopita kumekuwa na
manufaa mengi kati ya nchi ya Tanzania na Uingereza katika ushirikiano,
ubadilishanaji wa tamaduni na elimu, ikizingatiwa kuwa ndio mratibu
programu ya mafunzo kwa Watumishi wa Wizara ya Fedha kwa awamu zote tano
ilizojiwekea kuanzia yalipozinduliwa mwaka 2017.
Nao wanufaika
wa mafunzo katika vyuo mbalimbali vya Uingereza akiwemo Bw. Innocenti
Lema na Edwin Nalaila, wameishukuru Serikali kwa kufanikisha mafunzo
hayo na pia wameahidi kusoma kwa bidi na kutumia fursa zote
watakazozikuta ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa manufaa ya watanzania.
Wanufaika wa
Programu ya Mafunzo katika Vyuo mbalimbali vya Uingereza kwa ufadhili wa
UKaid awamu ya nne, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, ni pamoja na Bw.
Innocent Lema, Edwin Nalaila, Bi. Paulina Fungameza, William Mhehe na
Alpha Temu.
Serikali kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Uingereza (UKaid) walizindua programu ya mafunzo kwa
watumishi wa Wizara hiyo katika vyuo mbalimbali vya Ungereza kwa
ufadhili wa UKaid mwaka 2017, hii ni awamu ya nne ya utekelezaji tangu
programu hiyo ianzishwe ambapo watumishi 20 wamenufaika na mpango huo.
No comments :
Post a Comment