Akitangaza udhamini huo wenye
thamani ya Shilingi Milioni 40, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya
Klabu ya Gofu Lugalo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa NMB, Omary
Mtiga alisema udhamini wao unatokana na kutambua thamani ya michezo
ikiwemo gofu.
Mwenyekiti
wa Klabu ya Lugalo Brigedia Mstaafu Michael Luwongo (wa pili kutoka
kulia ) akipokea mfano wa hundi ya shilingi Milioni 40/- kutoka kwa Mkuu
wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Omari Mtiga, iliyotolewa
na Benki hiyo kwa ajlli ya udhamini wa michuano ya Gofu ya Mkuu
wa Majeshi. Kushoto ni Nahodha wa timu ya Gofu ya NMB, Michael Misabo na
kulia ni nahodha wa timu ya Gofu Lugalo, Captain Japhet Massawe.
Alisema ya kuwa, NMB kama taasisi
kinara ya kifedha nchini, inafurahishwa na aina ya
ushirikiano uliopo
kati yao na Klabu ya Gofu Lugalo inayoandaa michuano hiyo na kwamba
udhamini wao huo ni wa sita mfululizo tangia mwaka 2014 na unaakisi
nafasi ya Benki hiyo katika maendeleo ya michezo Tanzania.
“Tunafurahishwa na aina hii ya
ushirikiano baina yetu na waandaaji, ambao hauishii tu katika kudhamini
CDF Cup, bali pia unaoifanya NMB kuwa na nyota wengi wa gofu wanaounda
timu yetu, ambayo nayo itashiriki michuano hiyo,” alisema Mtiga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo,
aliishukuru NMB kwa namna inavyojitoa katika kusaidia ukuaji wa michezo
nchini, hasa CDF Cup inayoratibiwa na kuendeshwa na klabu yake. Alisema
wanatarajia kuwa na washiriki wengi mwaka huu, kutokana na mwitikio
aliouona, kwani hadi wanakabidhiwa hundi ya udhamini na NMB, kuna jumla
ya washiriki 110 waliojiandikisha, ikiwa imesalia wiki moja kabla ya
kuanza kwa michuano hiyo.
“Tayari washiriki 110 wamejisajili
hadi sasa kutoka klabu mbalimbali nchini, zikiwemo Lugalo, Dar
Gymkhana, Arusha Gymkhana, Zanzibar Gymkhana, NMB na nyinginezo, na
tunatoa wito washiriki wajitokeze zaidi na wazazi wawalete watoto wao
kushiriki,” alisema Luwongo.
Naye nahodha wa Klabu ya Gofu ya
NMB, Michael Misabo, alisema kuwa nyota wa timu yake wako tayari
kushindania na hatimaye kutwaa ubingwa wa CDF Trophy, kwani wamejiandaa
vya kutosha kuhakikisha wanafanya vyema katika kinyang’anyiro hicho.
“Katika CDF Cup 2020, NMB sio tu
wadhamini wakuu wa mashindano, bali pia ni washiriki tuliojiandaa
kuchuana na tunaingia tukiwa na uhakika wa kufanya makubwa na kutwaa
ubingwa wa jumla,” alisema Misabo mbele ya wanahabari waliohudhuria
hafla hiyo.
Kwa upande wake, nahodha wa Klabu
ya Gofu Lugalo, Japhet Masai, alisema kama timu wamejiandaa vya kutosha
na kwamba maandalizi ya jumla ya michuano yanaendelea vyema na kwamba
Ijumaa Septemba 18 kutafanyika utangulizi kwa nyota wa kulipwa kuchuana.
“Nyota wa kulipwa watatangulia
kuchuana Ijumaa ya Septemba 18, kisha ufunguzi rasmi Jumamosi na
kuhitimisha michuano Jumapili kwa nyota wa ngazi mbalimbal kutoana jasho
katika Divisheni za A, B na C kwa watoto, wanaume na wanawake, pamoja
na nyota wa ridhaa,” alifafanua.
No comments :
Post a Comment