Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikanyaga dawa maalum kabla
ya kuingia kwenye banda la kufugia kuku wa mayai kwenye shamba la Afro
Farm Ltd, anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko
katika wizara hiyo Bw. Stephen Michael.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe)
akizungumza na Mkurugenzi wa Afro Farm Ltd, Bw. Remen Kweka, mara baada
ya katibu mkuu kufika katika shamba hilo lenye kuku elfu ishirini ambao
wanazalisha mayai makasha (trays) zaidi ya 500 kwa siku.
Kutoka Kushoto; Katibu Mkuu Wizara
ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, Bi. Amillen
Kweka msimamizi wa Afro Farm Ltd, Mkurugenzi wa Afro Farm Ltd Bw. Remen
Kweka, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na
Uvuvi Bw. Stephen Michael na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya
Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.
Gabriel Bura, wakipata maelezo kutoka kwa Bw. Kweka namna shamba hilo
linavyotumia mashine kukusanya mbolea ya kuku, kusambaza chakula na
kukusanya mayai.
Baadhi ya kuku wanavyoonekana
wakiwa katika banda kwenye shamba la kufugia kuku wa mayai Afro Farm
ltd, lenye kuku elfu ishirini (20,000) ilhali likiwa na uwezo wa
kuhifadhi kuku elfu arobaini (40,000).
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe), akiwa na
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.
Stephen Michael (wa kwanza kutoka kushoto) pamoja na familia inayomiliki
Afro Farm Ltd, Bw. Remen Kweka (wa pili kutoka kulia) Bibi Amillen
Kweka mkewe (wa pili kutoka kushoto) na mtoto wao Bi. Emma Kweka (wa
kwanza kutoka kulia), wakionesha baadhi ya makasha (trays) ya mayai
kufuatia ufugaji wa kuku wa mayai unaofanywa katika shamba hilo ambao
unazalisha zaidi ya makasha 500 kwa siku.
Muonekano wa nje wa banda
linalotumika kufugia kuku wa mayai katika shamba la Afro Farm ltd
lililopo Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanajaro. (Picha na Edward Kondela –
Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
……………………………………………………………
Na. Edward Kondela
Watanzania
wametakiwa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini yakiwemo mayai ya
kuku ili kukuza sekta ya ufugaji ikiwemo ajira huku serikali ikisisitiza
mayai ya kuku wa kienyeji na kisasa ubora wake unatokana na
mchanganyiko wa vyakula anavyokula kuku.
Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro mara baada
ya kutembelea shamba la ufugaji kuku wa mayai Afro Farm Limited lenye
kuku elfu ishirini (20,000) wenye uwezo wa kuzalisha mayai zaidi ya
makasha (trays) 500 kwa siku, na kubainisha kuwa serikali imedhibiti
uagizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi na sasa mayai yapo mengi
nchini.
“Udhibiti
uingizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi soko sasa limepatikana na
niseme udhibiti huo siyo nguvu ya soda ni kwamba ni suala endelevu na
tutaendelea nalo na tunazidi kujipanga lakini sasa lazima tuhamasishe
watanzania kwamba wapende vya kwetu, ni suala ambalo kama wizara
tumejipanga mayai yanaleta afya bora na tunapoelekea uchumi wa viwanda
tunahitaji watu wenye afya bora.” Amefafanua Prof. Gabriel.
Kuhusu
wafanyabiashara wanaotozwa tozo ya shilingi elfu moja (1,000/=) kwa kila
kasha moja la mayai (tray) kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar Prof.
Gabriel amesema tayari kanuni zimeshabadilishwa na tozo imepungua hadi
shilingi mia moja (100/=) kwa kasha moja na kusisitiza wadau wa sekta ya
ufugaji kulipa kodi ili serikali iweze kufanya shughuli mbalimbali za
maendeleo.
“Nitoe
angalizo kwamba siyo vizuri sana mnapokuwa mnafikiria kuwa ifike mahali
kwamba msilipe gharama yoyote kwa serikali, hilo hapana ni lazima mlipe
kwa sababu mchango mnaotoa ndiyo unaojenga hospitali, barabara, shule
n.k.” Amesisitiza Prof. Gabriel.
Aidha Katibu Mkuu
Prof. Gabriel, ametoa wito kwa vijana kujiajiri katika sekta ya kuku
kwa kuwa ni sekta ambayo ni rahisi na yenye mahitaji makubwa kwa watu
kwa ajili ya nyama, mayai na mbolea huku akiwataka pia wafugaji wote
watambue kwamba lazima waangalie mnyororo wa mapato, gharama na faida
ili kupata kupata mafanikio makubwa na kuongeza ajira.
Pia amefafanua
kuwa ni vyema wadau wa ufugaji wa kuku wa mayai kufuata kanuni bora za
lishe ili waweze kuzalisha mayai bora badala ya kuwa na mayai mengi
yasiyo na ubora na kubainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina kuku milioni 83
na mayai bilioni nne huku mahitaji ya mayai yakizidi kuongezeka ndani
na nje ya nchi.
Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole
Gabriel amewataka pia wafugaji kutumia Dawati la Sekta Binafsi lililo
chini ya wizara hiyo kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo
ikiwemo ya mitaji na miongozo kwa kuwa dawati hilo ni kiungo kati ya
serikali na wadau wa sekta binafsi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Afro Farm Limited Bw. Remen Kweka amewataka vijana
kubadilisha fikra zao kwa kuhakikisha wanajifunza pindi miradi
mbalimbali inavyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini ili kujiwekea
mazingira ya kupata ajira na kubuni mitambo mbalimbali ya uzalishaji.
Bw. Kweka pia
amewaasa wadau wa ufugaji wa kuku katika miradi mikubwa kutumia Wakala
ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyo chini ya Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kupeleka sampuli za vyakula vya kuku ili kuhakikisha kuku
wanakula vyakula bora ambavyo vitatoa matokeo chanya ya upatikanaji
mayai yaliyo bora ambayo yanaweza kushindanishwa katika soko la
kimataifa.
Bi. Amillen Kweka
ambaye ni mke wa mkurugenzi wa shamba la Afro Farm amesema mradi huo
umewawezesha kusomesha watoto shule pamoja na kuwasaidia akinamama
kutokata tamaa na kuwafundisha juu ya ufugaji wa kuku wa mayai huku Bi.
Emma Kweka ambaye ni mtoto wa familia hiyo akiwaasa vijana kuwa na
shauku ya kujifunza ili kutafuta zaidi na kujiajiri kwa kuwa kujiajiri
ni jambo zuri ambalo unaweza kupangilia jambo lako katika muda unaotaka
na kusisitiza bidii na mipangilio ya kazi.
Shamba la ufugaji
kuku wa mayai la Afro Farm Limited kwa sasa lina kuku elfu ishirini
(20,000) na kuzalisha mayai makasha (trays) zaidi ya 500 kwa siku, huku
likiwa na uwezo wa kuhifadhi kuku elfu arobaini (40,000) na linatumia
mitambo ya kisasa katika kulishia kuku, kukusanya mayai pamoja na
mbolea.
Mwisho.
No comments :
Post a Comment