…………………………………………………………………
NA VICTOR MAKINDA
Shirika la Kikristu la Kuwahudumia
Wakimbizi (TCRS) mkoa wa Morogoro, limetoa misaada mbali mbali kwa watu
wanaoishi na ulemavu katika kata nne za Halmashauri ya wilaya ya
Morogoro mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa kutoa
misaada hiyo, Afisa Mwezeshaji wa TCRS mkoani humo, Gasper Werema,
alisema kuwa wao kama shirika wameguswa na changamoto mbali mbali
zinazowakabili watu wanaoishi na ulemavu na hivyo kuona umuhimu wa
kuwasaidia.
“Tumewapatia Radio ambazo zinatumia mwanga wa jua, sabuni na ndoo za kunawia maji.” Alisema Werema.
Werema aliongeza kusema kuwa watu
wanaoishi na ulemavu wana haki sawa na watu wengine ikiwa ni pamoja na
haki ya kupata habari, hivyo wameona ni vema kuwapatia radio ili waweze
kusikiliza habari na vipindi vya kuelimisha juu ya janga la corona na
masuala ya uchaguzi ikizingatiwa kuwa Taifa lipo katika kipindi cha
kampeni za uchaguzi mkuu.
Alisema kuwa misaada ya vifaa
hivyo umegharimu kiasi cha Shilingi 17.5 Milioni huku wenye ulemavu
389 wakinufaika na msaada huo sambamba na shule za msingi na vituo vya
afya.
Akizungumza mara baada ya kupokea
msaada huo,mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Hemed Mvuambaya, ambaye
ana ulemavu wa miguu mkazi wa kijiji cha Kibungo kata ya Mikese, alisema
kuwa analishukuru shirika la TCRS kwa kumpatia msaada wa Radio kwa kuwa
itakuwa faraja kwake na atapata fursa ya kujielimisha masuala mbali
mbali ya kijamii.
“ Sisi tunaoishi na ulemavu hasa
walemavu wa miguu, kutwa nzima tupo nyumbani. Tunapitwa na habari nyingi
na vipindi ambavyo vinatoa elimu. Msaada huu wa radio utanisaidia
kupata elimu juu ya sheria sera na haki zinazowahusu wenye ulemavu
lakini pia nitapata fursa ya kusikiliza vipindi vya michezo ambavyo
vitanipa burudani na faraja.” Alisema Hemedi.
Akizungumzia misaada iliyotolewa
na shirika la TCRS Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya na Morogoro,
Robert Manyerere, alilishukuru shirika hilo huku akitoa wito kwa watu
binafsi na mashirika mbali mbali kuwasiadia watu wanaoishi na ulemavu.
“ Sisi kama Halmashauri kwa niaba
ya Mkurugenzi tunalishukuru shirika la TCRS kwa kutoa misaada kwa kundi
hili la wenye ulemavu na maeneo mengine kama vile zahanati na shule za
misingi. Wito kwa jamii ya Kitanzania tuwasaidie wenye ulemavu ili
wasijione kama kundi lililotengwa katika jamii.”. Alisema Dkt
Manyerere.
No comments :
Post a Comment