Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria
Semakafu akizungumza na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya
Wananchi Same baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu chuoni
hapo ambapo ameutaka uongozi huo kutosajili fani ambazo hazina
wanafunzi.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria
Semakafu akitoa maelekezo ya namna ya kuboresha eneo la utoaji wa
mafunzo ya umeme wa magari kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya
Wananchi Same baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu chuoni
hapo.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya
miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi yaliyojengwa na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuongeza fursa za upatikanaji wa ujuzi
na maarifa kwa vijana wa Same.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo
ya Jamii Same, Edward Mdee akitoa taarifa ya chuo hicho kwa Naibu Katibu
Mkuu, Dkt. Ave Maria Semakafu alipofika chuoni hapo kwa ajili ya
kukagua maendeleo ya uboreshaji miundombinu na uendeshaji wa shughuli za
chuoni hapo.
………………………………………………………….
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Dkt. AveMaria Semakafu amevitaka Vyuo vya
Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kujikita katika kutoa mafunzo ya fani
zinazopendwa na zinazotoa ajira badala ya kuendelea kuwa na fani ambazo
hazina wanafunzi katika eneo husika.
Dkt. Semakafu ametoa agizo hilo
alipofanya ziara ya kukagua ukarabati na uendeshaji wa Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi Same kilichopo Mkoani Kilimanjaro ambapo amesema
ni vizuri vyuo vikajiimarisha kwenye utoaji mafunzo kwa fani zenye
wanafunzi wengi na
kuachana na zile zenye wanafunzi wachache.
“Kuanzia mwaka huu, kila chuo cha
wananchi kitafundisha fani ambazo zinahitajika katika maeneo husika kwa
maana ya kuwa na wanafunzi wa kutosha, hakuna chuo chochote kusajili
fani ambazo zina wanafunzi wachache ama chini ya kumi na mbili, Serikali
haiajiri walimu kufundisha wanafunzi wawili hivyo hakuna haja ya kuweka
fani ambazo hazina wanafunzi wa kutosha,” amesisitiza Dkt. Semakafu.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo
amesema mpango wa ‘Elimu haina mwisho’ unaotolewa katika vyuo hivyo ni
utaratibu wa kutoa fursa kwa watoto waliokatisha masomo kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii ili kuwasaidia kupata
elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuendelea na masomo na kuendesha maisha
yao pindi watakapohitimu hivyo wanapaswa kufundishwa kama wanafunzi
wengine bila kuwatenga.
Amesema Serikali iliamua watoto
hao wasome katika vyuo hivyo kupitia mfumo usio rasmi bila malipo yoyote
kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa nyingine ya kuendelea na masomo
na kuutaka Uongozi wa chuo cha Maendeleo Same kuwarudisha chuoni
wanafunzi wote walioacha masomo kwa sababu mbalimbali ili waweze
kumaliza masomo yao.
“Tumeanza programu hii kwa lengo
la kupata watoto wote walioacha shule na ndio maana unaona hata
wasichana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali
tumewarudisha katika mfumo huu ili waje waendelee na masomo na na wale
wenye watoto hata tuna shule za chekechea kwa ajili ya watoto wao,”
amesema Dkt. Semakafu.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Semakafu
amekagua miundombinu iliyokarabatiwa na kuboreshwa na Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia ambapo ameuagiza uongozi wa chuo hicho kufanya
marekebisho katika baadhi ya miundombinu ambayo haikukarabatiwa vizuri.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo
cha Maendeleo ya Wananchi Same, Edward Mdee ameishukuru Wizara kwa
ukarabati ambao umefanyika chuoni hapo, na kusema kuwa chuo hicho chenye
wanafunzi 301 kipo katika mkakati wa kuboresha utoaji wa mafunzo ili
kuhakikisha kinatoa vijana wenye ujuzi na maarifa yatakayowawezesha
vijana wa Same kujiajiri ama kuajiriwa.
No comments :
Post a Comment