
******************************
LEO Septemba15, 2020 Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa
demokrasia duniani katika kuadhimisha “Siku ya Kimataifa ya Demokrasia” –
“International Day of Democracy.”
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
lilipitisha siku hii Novemba 8, 2007 ili kuzikumbusha
Serikali juu ya
wajibu wake wa kukuza na kudumisha demokrasia na kuongeza uelewa wa umma
kuhusu suala hilo. Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa umoja huo inao
wajibu wa kutekeleza Azimio hilo kwa vitendo. Kauli mbiu ya maadhimisho
ya mwaka huu ni: “COVID-19: Inavyoangazia Demokrasia.”
Kauli mbiu hii imelenga
kuzikumbusha nchi wanachama juu ya umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi
ya gonjwa hatari la COVID-19 ambalo ni tishio siyo tu kwa afya ya jamii
bali pia ushiriki wao katika utawala wa nchi, hususan wakati wa kipindi
cha uchaguzi ambacho kinahusisha mikusanyiko mbalimbali ya wananchi.
Wakati siku hii ikiadhimishwa
leo, Tanzania inaendelea katika hatua ya kuhakikisha wananchi
wanashiriki katika kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua
viongozi wao katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Octoba, 2020. Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kuipongeza kwa dhati Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa
Corona 19 na hivyo kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika
hatua zote za uchaguzi huo.
Aidha, Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi na
wadau mbalimbali kuwa maradhi ya Corona 19 bado ni tishio katika nchi
mbali mbali duniani hivyo wana wajibu kuchukua tahadhari za kujikinga na
ugonjwa huo.
Kwa namna ya kipekee, Tume
inawahimiza wananchi kushiriki katika mikutano na majadiliano mbali
mbali ya kampeni na kusikiliza sera za viongozi ili kufanya uamuzi
unaofaa kwa maendeleo ya Taifa letu. Aidha Tume inawaasa viongozi
kutumia majukwaa ya kampeni kunadi sera zao na kujiepusha na lugha za
matusi na zenye kuhatarisha amani ya nchi yetu.
Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora inapenda kuwakumbusha wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha
wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mohamed Khamis Hamad
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
15 Septemba, 2020
No comments :
Post a Comment