Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
(aliyevaa miwani) akiwaongoza wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji
cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kuzindua zoezi la
uhimilishaji (kupandikiza ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).
Kaimu
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.
Stephen Michael akizungumzia kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha
Matebete Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya na namna wizara inayoshirikiana
na wananchi ili kuhakikisha wanapata mifugo bora.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Bi. Rahabu
Galahenga ambaye amehitimu diploma ya sheria. Prof. Gabriel amefika
katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa
ajili ya kuzindua kambi ya uhimilishaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati), akiwa
na wasichana wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya
Mbarali, Mkoani Mbeya waliohitimu masomo kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Kutoka kulia ni Bi. Naishiye Eliakimu amehitimu shahada ya ualimu, Bi.
Naumu Silomi amehitimu diploma ya uhandisi wa ndege, Bi. Rahabu
Galahenga amehitimu diploma ya sheria na Bi. Hawa Julius amehitimu
diploma ya ualimu.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
akimpongeza mfugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete
Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, baada ya ng’ombe wake kufanyiwa vipimo
kwa ajili ya kufanyiwa uhimilishaji.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel
akimpongeza mfugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete
Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, baada ya ng’ombe wake kufanyiwa vipimo
kwa ajili ya kufanyiwa uhimilishaji.
********************************
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema
serikali imelenga kuhakikisha wafugaji nchini wanakuwa na ng’ombe bora,
wenye kutoa nyama bora na maziwa mengi wanaopatikana kwa njia ya
uhimilishaji (kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).
Prof. Gabriel
amesema hayo katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya
wakati akizindua rasmi kambi ya uhimilishaji katika kijiji hicho kwa
wafugaji wa jamii ya kimasai na kuwataka waache kufuga kwa mazoea bali
wawe na ng’ombe bora na wenye tija huku akiwalenga zaidi akinamama
nchini kujikita katika ufugaji wa kisasa.
“Haya ni
mafanikio makubwa niwaombe akinamama wengine Tanzania waige mfano wa
kina mama wenzano wa jamii ya kimasai walioamua kufuga kisasa kwa kuwa
na ng’ombe bora hatuwezi kuendelea kwenye ufugaji wa zamani lazima
tufuge kisasa na uhimilishaji unafanyika kwa ng’ombe yeyote hata wa
kienyeji.” Amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel
akizungumzia faida za uhimilishaji amesema njia hiyo ya kumpatia ng’ombe
mimba kwa njia ya mrija ni muhimu katika kuendeleza ubora wa mifugo
hiyo ili kutengenzea mbari na kosaafu bora ya ng’ombe.
Amefafanua kuwa
uhimilishaji ni muhimu kwa kuwa mfugaji anaweza kuchagua ng’ombe
anayemtaka na ubora wake pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo hiyo kwa
ng’ombe dume kupanda ng’ombe wengi kwa wakati mmoja.
Ili kutoa hamasa
kwa wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo
Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi
amesema wafugaji watakaohimilisha ng’ombe elfu moja wa mwanzo wizara
itagharamia kama sehemu ya uzinduzi na uimarishaji wa kambi za
uhimilishaji.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo Bw.
Stephen Michael amesema wizara imekuwa ikifanya kazi karibu na wananchi
hali iliyofikia kuweka kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete
na kuwafanyia ng’ombe vipimo kabla ya kupandikizwa mbegu.
Naye Afisa Mifugo
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fadhil Chamwazi ameongeza kuwa
kambi za uhimilishaji zina malengo ya kuhamasisha wafugaji kutumia
huduma ya uhimilishaji na kuwajengea uwezo jamii ya wafugaji na wataalam
juu ya faida ya uhimilishaji.
Bw. Chamwazi
amesema zoezi hilo limeanza katika mwaka wa fedha 2019/20 na kwa mwaka
2020/2021 limezinduliwa mkoani Tabora na sasa katika Mkoa wa Mbeya
katika Kijiji cha Matebete na kubainisha kuwa vigezo vinavyoangaliwa kwa
ng’ombe kabla ya kupandikizwa mbegu ya uzazi kwa njia ya mrija,
wataalamu wanakagua afya ya ng’ombe pamoja na kuzingatia umri na
muonekano wake.
Nao baadhi ya
wafugaji wa jamii ya kimasai katika kijiji hicho wamefurahishwa na zoezi
hilo na kuiomba serikali kuendelea kuwapatia elimu zaidi na
kuwafahamisha namna bora zaidi za ufugaji wa ng’ombe bora wa kisasa ili
waweze kupata matokeo chanya katika ufugaji wao.
No comments :
Post a Comment