
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akitazama teknolojia ya kisasa ya kutumia chupa
kuzalisha mbegu za bora za migomba wakati alipotembelea kituo cha
utafiti TARI Dakawa wilaya ya Mvomelo jana.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akipokelewa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya
Wakulima Mkindo Eng.Grasian Kailembo jana alipokagua utendaji kazi wa
chuo hicho wilayani Mvomero.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akimwagilia mche wa muembe aliopanda jana alipotembelea
Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Ilonga na kuagiza vyuo vyote vya umma
nchini kujitegemea kibiashara kwa kuwa na mashamba darasa .
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya (kulia) akiongea na watumishi wa chuo cha mafunzo ya
wakulima Mkindo wilaya ya Mvomero .Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho
Eng.Grasian Kailembo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya (kulia) akitazama mche wa mchikichi wakati alipokagua
kitalu cha miche bora katika kituo cha utafiti TARI Ilonga wilaya ya
Kilosa jana.Kituo hicho kimefanikiwa kuotesha miche 600,000 ambayo
itagawiwa kwa wakulima wa mkoa wa morogoro lengo kuwezesha nchi
kujitosheleza kwa mafuta ya kula.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akiwa akijaribu kuendesha trekta alilokabidhi kwa kituo
cha utafiti wa kilimo TARI Ilonga jana ikiwa ni mkakati wa wizara
kuviwezesha vituo hivyo kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kwenye
mashamba yake.Jumla ya matrekta saba yamenunuliwa na wizara kupitia TARI
mwaka huu .

Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua mazingira ya chuo cha
mafunzo ya kilimo (MATI)Ilonga jana alipotembelea na kuahidi kuwa
seriklai katika mwaka huu itatoa shilingi Bilioni 70 kukarabati
miundombinu ya vyuo hivyo nchini.
( Habari na Picha na Wizara ya Kilimo)
……………………………………………………………..
Katika kuhakikisha Tanzania
inajitosheleza na uwepo wa wataalam bora wa kilimo serikali imepanga
kutumia shilingi bilioni 70 kuboresha miundombinu ya vyuo 14 vya mafunzo
ya
kilimo (MATI) nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana
(14.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati
alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa vyuo vya mafunzo ya Kilimo
Ilonga na TARI Ilonga wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro.
Alibainisha kuwa uwepo wa
mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya mafunzo ya
kilimo na vituo vyake yatawezesha kufanya mapinduzi katika kupata
teknolojia bora na mafunzo ya kilimo kuwezesha ukuaji wa sekta ya
kilimo.
“ Katika mwaka huu wa fedha
tumepanga kutumia shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kukarabati vyuo vyetu
vya kilimo vya serikali ikiwemo kuweka miundombinu wezeshi ya
kufundishia ,vifaa vya kufundishia na kuongeza wakufunzi na wanafunzi”
alisema Kusaya
Kusaya akiwa katika ziara hiyo ya
kikazi alibainisha mikakati saba ya wizara ya kilimo katika kuhakikisha
sekta ya kilimo nchini inakuwa na tija na kuchangia ukuaji wa uchumi na
kuongeza ajira kwa watanzania.
Alisema serikali inahitaji
kuwafundisha vijana wawe tayari kuwa maafisa ugani bora watakaofundisha
ujuzi pamoja na tekenolojia bora katika kwa vyuo vya umma na binasfi.
Mkakati wa kwanza wa wizara Kusaya
alisema ni kuhakikisha inakabiliana na upungufu wa wakufunzi 247
wanaotakiwa kwenye vyuo vyote 14 vya serikali kwa kuanzisha mpango wa
kutumia wahitimu wa vyuo vikuu vya kilimo kufanya mazoezi ya kazi (
interns) ili kupunguza tatizo.
Pili wizara ya kilimo itaanzisha
kanzi data ya wahitimu wa mafunzo ya kilimo kwenye vyuo vya umma na
binafsi ili kufahamu wapi walipo wanafunzi na kazi gani wanafanya ,lengo
serikali iweze kujua namna gani ya kuwaunganisha na vikundi vya
uzalishaji mali kupitia taaluma yao ya kilimo.
Tatu, wizara itaanzisha vituo
atamizi kwa ajili ya wanafunzi waliohitimu mafunzo ya kilimo kuwawezesha
vijana kutumia elimu yao kuanzisha shughuli za kilimo biashara
kivitendo ili waweze kujitegemea na kusaidia kufundisha vijana wengine
vijijini na mijini.
Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa
wanafunzi watakabidhiwa vitalu nyumba (green haouse) kupitia usimamizi
wa wakufunzi ili wazalishe mazao kwa kutumia elimu waliyoipata na kuwa
vituo hivi vitasaidia kuwafanya wanafunzi wengi kuwa mahili kwenye
uzalishaji mazao na kufundisha wakulima wengine.
“ Uwepo wa vituo atamizi utasaidia
wakulima wengi kupata mafunzo kwa vitendo toka kwa vijana wahitimu wa
kilimo watakaowezeshwa na wizara kufanya kilimo biashara hali
itakayoongeza ajira na tija katika uzalishaji wa mazao nchini”
alisisitiza Kusaya.
Kusaya alitaja mkakati wa nne ni
kuhakikisha vyuo vya mafunzo ya kilimo vinatoa teknolojia ya kisasa kwa
kutumia mtandao ndio maana mwisho mwa mwezi Agosti alikabidhi kompyuta
05 kwa vyuo vyote 29 vya kilimo vya umma na binafsi na kuwa lengo kila
chuo kitapatiwa kompyuta 30 ifikapo mwisho mwa mwaka huu.
”Tunataka kuwa na mfumo wa
kufundisha kielektoni (e-learning) ili kuunganisha vyuo vyote kutumia
vifaa vya kompyuta na kuleta mapinduzi katika fani ya kilimo”
alielekeza Kusaya.
Mkakati wa tano wa wizara ni
kuhakikisha vyuo vyote vinatumia ardhi iliyopo kuzalisha mali na
kufundisha wanafunzi kupitia mashamba darasa na kuwa serikali itatoa
trekta moja kwa kila chuo cha mafunzo ya kilimo cha serikali ili kuweka
mazingira rafiki na waweze kujiendesha kibishara.
“ Vile vyuo vinavyojihusisha mfano
na uzalishaji wa mpunga au ngano tutawapelekea zana zinazoendana na
mafunzo wanayotoa kwa wanafunzi ili waongeze tija na uzalishaji na
hatimaye wapate mapato ya kujitegemea kiuchumi” alisisitiza Kusaya.
Sita, wizara ya kilimo itatoa
magari kwa vyuo vyote 14 vya mafunzo ya kilimo vya serikali na kugawa
pikipiki tatu ili kurahisisha upatikanaji wa usafiri na utoaji huduma.
“ Tayari tumepeleka pikipiki sita
katika vyuo Inyara Mbeya, Igurusi Mbeya na Ukirigulu Mwanza kila
kimoja pikipiki mbili ili kuviwezesha kutekeleza majukumu yake .Awamu
ya pili itahusisha kupeleka pikipiki kwenye vyuo vingine 11” alisisitiza
Kusaya.
Saba , wizara ya kilimo ni
kukarabati miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya kilimo ili majengo na
vifaa vya kufundishia yawe ya kisasa na kusaidia kuboresha ufundishwaji.
Mpaka sasa Kusaya alisema
amekwishatembelea vyuo vya mafunzo ya kilimo 12 kati ya 14 tangu
alipoteuliwa mwezi Machi mwaka huu ambapo amegundua kuwa kuna uhitaji
mkubwa wa kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya
kilimo nchini.
Katika hatua nyingine Kusaya
alitembelea na kukagua utendaji kazi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI
Dakawa wilaya ya Mvomero na kukipongeza kituo hicho kwa kuongeza
uzalishaji mbegu bora za mpunga .
“ Nawapongeza TARI Dakawa kwa
kuongeza uzalishaji mbegu bora za mpunga toka tani 75.6 mwaka 2015/16
hadi tani 93.7 mwaka 2019/20 hali iliyosaidia kukuza tija na uzalishaji
mpunga nchini” alisema Kusaya
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt.Geofrey Makamilo alisema taasisi
hiyo inaendelea kujikita kuhakikisha utafiti na upatikanaji mbegu bora
za mazao unaimarika na kuwa tayari mwaka huu wamepokea Shilingi Bilioni
1.4 kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za michikichi ili kugawa kwa
wakulima.
Dkt.Mkamilo alibainisha pia TARI
wamepokea Shilingi Bilioni 1.76 mwaka huu 2020 kwa ajili ya kuzalisha
mbegu begu bora za zao la mkonge mkoani Tanga.
“ Jumla ya hekta 30.2 za mbegu ya
mkonge zimelimwa katika kituo cha utafiti Mlingano na miche milioni
2.4 imekwisha zalishwa na itagawiwa kwa wakulima katika mikoa 17
inayolima mkonge nchini” alisema Dkt.Mkamilo.
Katibu Mkuu Kusaya alitembelea pia
kituo cha utafiti wa kilimo TARI Ilonga wilayani Kilosa na kujionea
kazi ya uzalishaji miche bora ya michikichi ipatayo 600,000
itakayogawiwa kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro ili kupanda.
Alikipongeza kituo hicho na kutoa
wito wa kuongeza kasi ya kuzalisha mbegu bora ya michikichi aina ya
Tenera yenye kutoa mafuta mengi ili kutimiza agizo la Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa la kuifanya nchini iondokane na utegemezi wa mafuta ya kula
toka nje ya nchi.
“Tanzania kwa mwaka tunatumia
shilingi bilioni 443 kuagiza mafuta ncje ya nchi wakati tunayo ardhi
inayofaa kwa kilimo cha mazao ya mafuta kama michikichi, alizeti na
karanga. TARI endeleeni kuzalisha miche mingi bora ya michikichi kwa
ajili kugawa kwa wakulima” alisema Kusaya
Kusaya alisema wizara ya Kilimo
itaendelea kuhakikisha mahitaji ya kifedha na vifaa kama matrekta kwa
taasisi ya utafiti wa kilimo ikiwemo upatikanaji wa maabara bora kwa
kila kituo kwa ajili ya kupima afya ya udongo na kushauri wakulima
zinapatikana.
Mwisho
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MOROGORO
15.09.2020
No comments :
Post a Comment