Mmoja
wa washiriki (aliyesimama) wa kikao kazi cha siku mbili kilichojadili
na kutoa mapendekezo ya kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa
Masuala ya Jinsia katika Utumishi wa Umma akitoa mchango wake katika
kikao kazi hicho, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu
na Nyaraka za Taifa jijini DODOMA jana jioni.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa
kikao kazi cha siku mbili kilichojadili na kutoa mapendekezo ya
kuboresha Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika
Utumishi wa Umma, mara baada ya kufunga rasmi kikao kazi hicho
kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa
jijini DODOMA jana jioni.
……………………………………………………………………..
Na. Aaron Mrikaria-Dodoma
Serikali
imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Ujumuishaji wa Masuala ya Jinsia katika
Utumishi wa
Umma ambao utatoa maelekezo ya namna ya kujumuisha masuala
ya kijinsia mahala pa kazi na kujenga mazingira bora na wezeshi kwa
makundi mbalimbali kwenye taasisi za umma, ili mwongozo huo uwe ni
chachu ya kuongeza tija kiutendaji kwa Watumishi wa Umma na Serikali kwa
ujumla.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael wakati akifunga
kikao kazi cha siku mbili kilichohudhuriwa na Wakurugenzi wa Wizara zote
kilichojadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha rasimu hiyo, kikao
hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za
Taifa jijini DODOMA.
Dkt.
Michael amewasititiza waajiri kuwa, pendekezo la urithishanaji madaraka
kuzingatia suala la kijinsia lipewe umuhimu mkubwa katika utekelezaji
wake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata fursa kujumuishwa
kwenye mipango ya mafunzo ili kujengewa uwezo kiutendaji.
Licha ya
kuafiki pendekezo la kutilia mkazo haja ya wanawake kupewa kipaumbele
katika nafasi za uongozi na kuwekewa mazingira wezeshi katika
utekelezaji wa majukumu yao mahala pa kazi, Dkt. Michael pia amehimiza
umuhimu wa rasimu hiyo kuyawezesha makundi yote kutekeleza wajibu wao
kwa ufanisi katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Dkt.
Michael awetaka viongozi katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanabaini
watumishi wenye vipaji maalum kutoka makundi anuai na kuviendeleza
vipaji hivyo, pamoja na kuangalia namna ya kuanzisha vituo vya malezi
kwa watoto katika majengo ya Ofisi za Umma ili mtumishi anayenyonyesha
aweze kutumia muda wake kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya
kikazi.
Naye,
Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amesema tofauti na
Mwongozo wa mwaka 2010, rasimu hii inayoboreshwa imezingatia masuala ya
jinsia na usimamizi wa rasilimaliwatu, hivyo muongozo huu ukiidhinishwa
rasmi kutumika utakuwa ni mahususi kuratibu ujumuishwaji wa masuala ya
jinsia katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwenye Utumishi wa Umma.
No comments :
Post a Comment