Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru (katikati)
akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari Agosti 31 mwaka huu
kuhusu kuongezwa kwa muda katika dirisha la maombi ya mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/21. Kushoto ni
Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Joseph
Kimaro na kulia ni Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta
Tanzania (TPC) Mwanaisha Said.
(PICHA NA BODI YA MIKOPO- HESLB)
…………………………………………………………………..
- Maombi 92,947 yapokelewa na kusajiliwa
Na Mwandishi Wetu,HESLB
DAR ES SALAAM
BODI ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kufungwa kwa
dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020
ambapo hadi kufikia
leo Septemba 10, 2020 imepokea na kusajili jumla ya
maombi ya wanafunzi 92,947.
Taarifa
iliyotolewa leo Alhamisi (Septemba 10, 2020) Jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mtendaji wa (HESLB), Abdul-Razaq Badru imesema mfumo wa
maombi hautaweza kuruhusu usajili wa maombi mapya ya waombaji isipokuwa
kwa waombaji 7,500 waliopo mtandaoni ambao hawajakamilisha maombi hayo.
Badru amesema
HESLB ilifungua dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa muda
wa siku 40 kuanzia tarehe 21 Julai mwaka huu, ambapo hata hivyo
kufuatia maoni na maombi ya wazazi, walezi na wanafunzi iliongeza muda
wa siku 10 hadi leo Alhamisi Septemba 10, 2020 ili kutoa fursa kwa
waombaji kukamilisha maombi hayo.
“Leo Alhamisi
(Septemba 10, 2020) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa
njia ya mtandao, litafungwa rasmi. Baada ya muda huo, usajili mpya kwa
ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa’’ alisema Badru
AIdha, Badru
alisema Oktoba Mosi mwaka huu HESLB itaanza zoezi la uchambuzi wa maombi
hayo na baadaye itaorodhesha maombi yote yenye mapungufu na
kuwatangazia waombaji husika kwa ajili ya kurekebisha kasoro
zilizojitokeza.
Akifafanua zaidi, Badru aliwataka wazazi, walezi na wanafunzi kuendelea kufuatilia vyanzo rasmi ikiwemo tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz)
kuhusu taarifa muhimu na orodha ya watakaopangiwa mikopo kwa mwaka wa
masomo 2020/2021 kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa kitaaluma (academic
almanac) ya mwaka huu.
Serikali kupitia
HESLB, imetenga kiasi cha TZS Bilioni 464 kwa ajili ya
wanafunzi 145,000, ambapo kati yao wanafunzi wanufaika 54,000 watakuwa
wa mwaka wa kwanza na 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na
masomo.
No comments :
Post a Comment