Dar es Salaam:
Wateja wa Vodacom M-Pesa
takribani milioni 8, kuanzia leo watapata sehemu ya faida ya shilingi
bilioni 3.5 ikiwa ni gawio kutoka kwenye akaunti ya M-Pesa Trust.
Kampuni ya
Vodacom Tanzania PLC imetangaza kwamba kuanzia leo wateja
wake wa M-Pesa watapata sehemu yao ya gawio hilo lililopatikana kama
faida ya matumizi ya huduma hiyo.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Mkurugenzi wa M-Commerce Epimack Mbeteni alisema, “tuna shauku
ya kugawana faida hii na wateja wetu kwani wao ndio sababu ya mafanikio
ya huduma ya M-Pesa. Huduma ya M-Pesa imechangia maendeleo lukuki ya
watanzania na mpango huu umedhamiria kuendelea kuwapa wateja wetu faida
zaidi. Wateja wote wa Vodacom ambao wamekuwa wakitumia M-Pesa kuanzia
Januari mosi hadi Machi 31 mwaka huu watafaidika na bonus hii ya
shilingi bilioni 3.5 ambayo itagawiwa moja kwa moja kupitia M-Pesa”.
Kuanzia sasa wateja wa Vodacom
wanaweza kutuma SMS ya neno KIASI kwenda namba 15300 ili kujua kiwango
gani cha faida watapokea. Baada ya kupata gawio hili, wateja wa M-Pesa
wanaweza kukomboa faida hiyo kwa kuitoa kama fedha taslimu, kununua muda
wa maongezi, vifurushi au kulipia bili.
“Kiasi ambacho mtu atapokea kama
sehemu ya faida hiyo itategemea na idadi ya miamala aliyokuwa akifanya
kwa kipindi nilichotaja hapo juu. Shughuli hizo ni kama miamala ya
kuhamisha fedha, malipo ya bili mbalimbali au manunuzi ya muda wa
maongezi. Napenda kuwahimiza wateja wetu kutuma SMS ili kujua ni kiasi
gani cha gawio hili wanastahili kupokea,” alisisitiza Mbeteni huku
akiongeza kwamba mpaka sasa Vodacom Tanzania PLC imeshagawa faida ya
jumla ya shilingi bilioni 133 kwa wateja wa M-Pesa.
M-Pesa ina umiliki wa soko wa
asilimia 39 na inaongoza kwa kuwa huduma ya fedha za mkononi inayotumiwa
na watanzania wengi zaidi ambao wanafanya miamala ya hadi Shilingi
bilioni 100 kwa siku. “Tumewekeza vilivyo katika M-Pesa ndani ya miaka
kumi na mbili iliyopita na sasa huduma imekuwa na ufumbuzi wa kibunifu
unaokidhi mahitaji ya watanzania kupitia bidhaa mbalimbali kama vile
M-Koba, M-Pawa, Halal Pesa M-Pesa MasterCard na nyingine nyingi.
Tunaendelea kuwa na nia ya kuboresha huduma hii kwa njia ya ubunifu huku
tukishirikiana na makampuni pamoja na wavumbuzi mbalimbali ili
kuendesha ajenda ya ujumuishwaji wa kifedha nchini,” alimaliza Mbeteni.
No comments :
Post a Comment