Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya akikagua skimu ya umwagiliaji Ruaha Mbuyuni iliyoharibiwa
na mafuriko mwanzoni mwa mwaka huu kufuatia mtoa Ruaha mdogo kuacha njia
yake ya asili.
Ukaguzi wa
banio la skimu ya umwagiliaji Ruaha Mbuyuni wilaya ya Kilolo
lililoharibiwa na mafuriko.Pichani Katibu Mkuu akiangalia jinsi mto
Ruaha mdogo ulivyoacha njia na kusababisha maji kuharibu miundombinu ya
mashamba jana alipofanya ziara.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya (kushoto) akiangalia ramani ya skimu ya umwagiliaji Magozi
iliyoharibiwa na mafuriko mwaka huu jana alipotembelea wilaya ya Iringa
ambapo ameahidi kutoa shilingi milioni 350 kufanya ukarabati wa skimu
nne kwenye wilaya hiyo. Alishika fimbo ni mkulima Fundi Mihayo wa kijiji
cha Luganga.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshikwa mkono kuvuka toka mtoni alipokagua eneo
la mto Ruaha kijiji cha Luganga wilaya ya Iringa jana.Skimu hiyo
yaumwagiliaji ilihabiwa na mafuriko kufuatia mto Ruaha mdogo kuhama
njia.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya (kulia) akiongea na wakulima wa skimu ya umwagiliaji Ruaha
Mbuyuni wilaya ya Kilolo jana alipokagua uharibifu uliotokana na mto
kuhama njia.Wizara imetoa shilingi milioni 60 kupitia Tume ya
Umwagiliaji kukarabati skimu hiyo kuanzia wiki ijayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya (kulia) akifurahi jambo alipokuwa akiongea na Afisa Kilimo
Mstaafu Mzee Dkt.Jairos Mapepele mkazi wa kijiji cha Ruaha Mbuyuni jana
alipotembelea kujionea uharibifu wa skimu hiyo ya umwagiliaji. Wizara
ya Kilimo itatoa shilingi milioni 60 mapema wiki ijao ili kurejesha mto
Ruaha kwenye nia yake ya asili kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Wakulima
wa kijiji cha Luganga wilaya ya Iringa Vijijini wakivuka mto Ruaha mdogo
jana kwenda upande wa pili ili kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya (hayupo pichani) alipokagua uharibifu wa skimu ya
umwagiliaji kufuatia mafuriko mwanzoni mwaka huu.
( Habari na Picha Wizara ya Kilimo)
……………………………………………………………………………..
Serikali itatoa shilingi milioni
410 kwa ajili ya kukarabati skimu za umwagiliaji mashamba yaliyoharibiwa
na mafuriko mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mto Ruaha kuacha njia
yake ya asili.
Kauli hiyo imetolewa jana
(04.09.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya
ziara ya kukagua uharibifu wa skimu za umwagiliaji za Pawaga na Ruaha
Mbuyuni mkoani Iringa.
Kusaya amezitaja skimu ambazo
zitanufaika na fedha hizo kuwa ni Mkombozi, Mlenge, Luganga na Magozi
wilaya ya Iringa zitakazopewa shilingi milioni 350 na skimu ya
umwagiliaji Ruaha Mbuyuni itapewa shilingi milioni 60.
“Imenisukuma kuja hapa Pawaga
kuona hali halisi ya uharibifu wa skimu zetu 4 za umwagiliaji
zilizoharibiwa na mafuriko na kuwa Wizara ya Kilimo italeta shilingi
milioni 350 mapema wiki ijayo ili kukarabati miundombinu “alisema Kusaya
Akiwa katika skimu ya Mkombozi ,
Mlenge, Magozi na Luganga wilaya ya Iringa Katibu Mkuu huyo alisema
atatuma wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji pamoja na mitambo
(greda) kurekebisha miundombuni hiyo iliyoharibiwa kufuatia mto Ruaha
mdogo kuacha njia yake ya asili.
“ Nahitaji jumatatu tarehe
07.09.2020 mitambo iwepo hapa Pawaga na wataalam ili kazi ya kurejesha
mto ianze na wakulima wapate maji kwenye mashamba yao” alisema Kusaya.
Kusaya aliwaambia wakulima wa
mpunga kwenye skimu hizo kuwa serikali ya awamu ya tano ipo bega kwa
bega kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinakuwa bora na kufanya kazi
mwaka mzima,hivyo wakulima watoe ushirikiano kwa Tume kufanikisha
ukarabati wa skimu.
Aliwahakikishia wakulima wa mpunga
kwenye skimu hizo kuwa hakuna atakayechangishwa fedha bali serikali
ndio itatoa fedha hizo kukarabati miundombinu ya umwagiliaji
iliyoharibika na kuwa jukumu la wananchi ni kushirikiana na wataalam
kwa kazi ndogo ndogo kama kubeba mawe na mchanga kwenye maeneo ya kazi.
“ Nataka ndani ya wiki moja
kuanzia sasa wataalam wa Tume ya Umwagiliaji mfanye kazi ya kuurejesha
mto Ruaha mdogo kwenye njia yake ,vifaa na mitambo ipo .Wakulima
wanachohitaji ni maji yafike kwenye mashamba yao haraka” aliagiza Kusaya
Akiwa katika skimu ya umwagiliaji
Ruaha Mbuyuni Katibu Mkuu Kusaya alijionea jinsi mto Ruaha ulivyoacha
njia zaidi ya mita 100 na kufanya banio kutokupitisha maji na wakulima
kushindwa kulima zaidi ya hekta 450 msimu huu.
Aliwahakikishia wakulima hao kuwa
Wizara ya Kilimo itafanya kazi ya kurejesha mto kwenye njia yake ya
asili ili maji yafike kwenye mashamba ya wakulima kwa kuwa mto huo ndio
tegemeo la wakulima kuzalisha mazao ya chakula yakiwemo mpunga,mahindi
na mazao ya mboga mboga (horticulture).
Kusaya ameahidi kuwa baada ya wiki
mbili atarudi wilaya za Kilolo na Iringa kukagua maendeleo ya kazi ya
kurejesha mto kwenye njia yake na kuwa amezitaka halmashauri hizo
kushirikiana na Wizara kukarabati miundombinu hiyo mapema.
Akizungumza kwenye ziara hiyo
mkulima Fundi Mihayo wa kijiji cha Luganga wilaya ya Iringa aliishukuru
Serikali kwa kuguswa na matatizo ya wakulima na kuchukua hatua.
Alisema katika mvua nyingi
zilizonyesha mwezi Januari mwaka huu zilisababisha mafuriko yaliyoharibu
skimu hivyo kusababisha mazao kuharibika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bashiri Mhoja alisema mwaka huu wakulima
walipata hasara kwa kuzalisha asilimia 2 tu ya zao la mpunga kutokana
na miundombinu ya skimu za umwagiliaji kuharibiwa na mafuriko hivyo
ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa hatua ya kutoa fedha na wataalam
kukarabati.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ruaha
Mbuyni wilaya ya Kilolo Hamis Matabazi alisema wanakijiji wapo tayari
kutoa ushirikiano kwa serikali kufanikisha urejeshaji mto Ruaha mdogo
kwenye njia yake kwani wana uhitaji mkubwa wa kuendelea na kazi ya
uzalishaji mazao.
“ Tunaomba Katibu Mkuu utufikishie
salamu zetu kwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kusikiliza kilio chetu
wananchi wa Ruaha Mbuyuni na kuleta fedha za kukarabati skimu yetu hii”
alishukuru mwenyekiti wa kijiji chicho .
Katibu Mkuu Kusaya pia alitoa wito
kwa wakulima wa Kilolo na Iringa kutunza mazingira kwa kupanda miti
kandokando ya mto Ruaha ili kulinda kingo za mto zisiharibiwe na mvua.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
IRINGA
05.09.2020
No comments :
Post a Comment