Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji akifunga mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro yaliyofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara akipokea cheti kutoka kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji baada ya kufunga mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala, Halmasauri ya Wilaya ya Chemba, Bw. Martin Ndilanha ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara akitoa neno la shukrani kwa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji mara baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji kufunga mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
*************************************
James Mwanamyoto – Dodoma
Tarehe 27 Septemba, 2020
Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 108 waliohitimi Mafunzo ya siku 12 ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara wametakiwa kukamilisha usahihishaji wa
taarifa za watumishi zilizopo kwenye mfumo wa sasa ili ziweze kuingizwa katika mfumo mpya, kwani mfumo mpya hautoruhusu kuingiza taarifa ambazo sio sahihi na zisizokamilika.Maelekezo hayo yametolewa jana jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Cosmas Ngangaji wakati akifunga mafunzo hayo yaliyokuwa na lengo la kuboresha utendaji kazi na usimamizi wa rasilimaliwatu na mishahara.
Bw. Ngangaji amesema, baada ya kukamilika kwa mafunzo haya na kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huu mpya, Serikali inatarajia mfumo mpya utatumika kutatua kero za watumishi kwa ufanisi na kwa haraka zaidi ikiwa ni pamoja na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi.
Bw. Ngangaji ameongeza kuwa, mfumo mpya utaongeza uadilifu kiutendaji kwani umewezeshwa kurekodi matukio yote yatakayokuwa yakifanywa na Maafisa waliopewa dhamana ya kutumia Mfumo huo.
“Serikali kupitia mfumo huu itakuwa ikifuatilia na kujua ni Afisa yupi amefanya nini au amekusudia kufanya nini, wapi na muda gani? Bw. Ngangaji amefafanua.
Aidha, Bw. Ngangaji amesema mfumo mpya utaimarisha uwajibikaji na kuwawezesha watumishi kufuatilia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi yanayowahusu kupitia simu na barua pepe hivyo, kuongeza uwajibikaji na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea.
“Watumishi wa Umma watakuwa wakipata taarifa na kujua kama kazi iliyofanyika bado ipo kwa Afisa Utumishi, Mwajiri au imeshatumwa UTUMISHI kwa ajili ya kuidhinishwa,” Bw. Ngangaji amesisitiza.
Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Bw. Martin Ndilanha kwa niaba ya washiriki wa mafunzo amemhakikisha Bw. Ngangaji kuwa, wamepata mafunzo bora ya mfumo mpya na kuwa wabobezi katika kuutumia ili kuondoa kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma nchini.
Bw. Ndilanha amesema, Mfumo huo mpya ulioboreshwa unapunguza uzalishaji wa madeni kwa Serikali, unarahisisha na kupunguza gharama za uandaji wa bajeti ya Serikali hivyo wako tayari kuutumia ipasavyo.
Serikali imepanga kuanza matumizi rasmi ya mfumo huu mpya mwezi Novemba, 2020 baada ya kukamilisha mafunzo kwa makundi manne ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2020.
No comments :
Post a Comment