**************************************
NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA kuhakikisha nchi ya Tanzania haingii katika mtego wa
matumizi ya bidhaa zinazotokana Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO)
wanadau wameshauri kuwepo na mjadala wa
kitaifa na kutolewa elimu
kuanzia shule ya msingi kuhusu madhara yake.
Wadau hao wanakuja na ushauri huo ambapo kwa sasa dunia nzima
pamoja na kuwepo mikataba, sheria, kanuni na miongozo ya uzalishaji na
matumizi ya bidhaa hizo wanapiga vita kwa kile kinachodaiwa bidhaa za
GMO kuwa na madhara kwa viumbe hai.
Wakichangia kwenye warsha ya siku moja iliyofanyika jijini
Dar es Salaam na kushirikisha wakulima wa kilimo hai na wanaharakati
wanaopambana na matumizi ya GMO wadau hao walisema mapambano dhidi ya
bidhaa hizo yanahitaji elimu na mjadala wa kitaifa.
Abdallah Mkindi kutoka Tanzania Alliance for Biodiversity
(TABIO), alisema kuruhusu GMO nchini ni kurudisha nyuma mkulima kwa kuwa
mbegu hizo sio endelevu.
Alisema wanatarajia mwishoni mwa mwaka huu jijini Dodoma
wataandaa tukio ambalo litajikita kwenye kuzungumzia chakula na mbegu
ili kusaidia jamii kuelewa kwa kina madhara ya GMO.
Mkindi alisema TABIO
imekuwa ikishirikiana na mashirika ya ndani na nje kuhakikisha wakulima
wanazingatia kilimo hai ambacho kinatumia mbegu asili na kuachana na
mbegu ambazo sio za kudumu.
“Sisi TABIO
tumedhamiria kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha GMO
haingii nchini kwa njia yoyote kwani ushahidi upo kuwa bidhaa na mbegu
zake zina madhara kwa binadamu na viumbe hai wengine,” alisema.
Alisema hoja ya watu
wa GMO imejikita katika ukame, wadudu vamizi na mabadiliko ya tabia nchi
hali ambayo inaweza kudhibitiwa kwa kuwepo elimu ya kutunza mbegu asili
kama ilivyokuwa zamani na kuhamasisha utunzaji mazingira.
Mwakilishi kutoka
Kundi la Kupinga Matumizi ya GMO Tanzania, Albert Kamala alisema iwapo
hakutakuwa na kauli moja baina yao kuna dalili ya jamii kuangamia siku
chache zijazo.
Kamala alisema wao
wameamua kupinga GMO kwa kuwa wanajua na kuona madhara yake kuanzia
shambani hadi majumbani hivyo wanaamini Serikali inapaswa kuunga mkono
kwa nguvu zote ili utekelezaji uonekane.
“Tumeamua
kuwakutanisha hapa leo ili tuweze kuzungumza lugha moja kati ya sisi
wanaharakati wa kupinga GMO na wakulima na baadae tupeleke ujumbe mmoja
Serikalini ili hatua zichukuliwe kwani dalili sio nzuri iwapo tutaruhusu
kilimo na matumizi ya bidhaa hizo katika nchi,” alisema.
Naye Sabrina
Masinjila alisema utafiti unaonesha kuwa mbegu za GMO zimeendelea kuwa
na athari zaidi kuliko faida kwa wakulima hivyo zinapaswa kupingwa kila
mahali.
“Inasemekana mbegu
hizo zinaimarisha wadudu vamizi, lakini kilimo hicho kinataka nafasi
sana jambo ambalo ni changamoto kwa wakulima wadogo hata huko katika
nchi ambazo zilianza zimeanza kuacha kwani hasara ni kubwa zaidi,”
alisema.
Aidha, alisema
taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa mazao yatokanayo na GMO yamekuwa
yakichangia ongezeko la saratani duniani hivyo hakuna sababu ya kuunga
mkono.
Masanjila alisema
Tanzania inapaswa kuwa na mjadala wa kitaifa ambao utatoa muongozo wa
nini cha kufanyika ili kutoka katika janga hilo.
Bonaventure Charles
Mwanharakati wa kupinga GMO kutoka Arusha aliomba Watanzania wapaze
sauti ili kuhakikisha mbegu NA bidhaa za GMO hazipati nafasi nchini.
Mwanaharakati huyo
alisema juhudi zielekezwe kwenye matumizi ya mbegu asili ambazo
zinaonesha kuwa na matokeo chanya kwa miaka mingi.
“Pamoja na kupaza
sauti pia kuwepo mashamba darasa ambayo yatasaidia wakulima kutambua
mbegu asili ni zipi na GMO ni zipi kwani wakati mwingine ni changamoto
kutambua,” alisema.
Ofisa Miradi wa Umoja
wa Walima Matunda na MbogaMboga Zanzibar (UWAMWIMA) Khamis Issa
Mohammed, alisema mjadala wa kitaifa utasaidia jamii kutambua thamani ya
chakula na mbegu asili kwenye maisha yao tofauti na ilivyo sasa.
Mohammed alisema
ufanisi wa mjadala huo unatakiwa kuhusisha makundi yote muhimu ambao ni
wakulima, wanaharakati, waandishi wa habari, wanadau wa maendeleo na
Serikali ili kuwa na mtazamo mmoja.
Mwenyekiti wa Umoja
wa Waandishi Mkoani Dar es Salaam (DCPC), Irene Mark alisema mapambano
ya GMO yanaweza kufanikiwa iwapo elimu itatolewa kuanzia elimu ya
msingi.
Aidha aliwataka wadau
kuwatumia waandishi wa habari kuanzia ngazi za awali katika mapambano
hayo na sio kusubiri kuwapa taarifa ya utekelezaji.
“Mimi naamini
mapambano haya yanahitaji kujikita kuanzia elimu ya msingi, ila naomba
msitutumie kuripoti mliochokiona tuwekeni kwenye mipango yenu kuanzia
ngazi ya awali tutafika pamoja,” alisema.
Kwa upande wake
Mtafiti wa Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI -Dakawa),
John Joseph alisema changamoto ya GMO inahitaji uwanda mpana wa mjadala
ili kuwa kitu kimoja.
Alisema TARI-Dakawa wanaendelea na utafiti wa mbogamboga asili hivyo ni imani yake suluhu ya mbegu zenye mashaka itapatikana.
Akiwasilisha mada
katika warsha hiyo ya siku moja Mwanasheria kutoka Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira, Isakwisa Mwamukonda alitoa rai kwa
wanaharakati wanaopinga GMO kufanya utafiti wa kina kuhusu mbegu na
bidhaa kwa kuwa ina faida na hasara.
Mwamukonda alisema
iwapo bidhaa na mbegu GMO zipo nchini ni wazi kuwa zipo kisheria kwa
kuwa sheria zetu zinaruhusu ila kwa kufuatwa hatua mbalimbali muhimu.
“Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Bioaniwai (1992), Mkataba Mdogo wa Cartagana (2002), Mkataba wa Nagaya.
Sera ya Taifa
Mazingira (1997), Sera ya Taifa ya Biotechnolojia ya Kisasa (2009), Sera
ya Kilimo ya (2019), Sheria ya Mazingira ya (2004) na Sheria za
Kisekta,” alisema.
Mwanasheria huyo
alisema katika kukabiliana na GMO nchini ni lazima wafanye utafiti wa
kina ambao utawezesha watunga sera kuelewa na kufanya maamuzi sahihi.
Mmoja wa Waandaaji wa
warsha hiyo, Austin Makani alisema warsha hiyo imewapa muongozo wa nini
cha kupeleka Serikalini ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya hofu ya
bidhaa na mbegu za GMO nchini.
“Kwa ujumla
tunashukuru na tumepokea michango yote ambayo imetolewa na tutahakikisha
inafika sehemu husika kwa hatua zaidi,” alisema.
No comments :
Post a Comment