Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na
Biashara wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi akizungumza wakati wa Mkutano
na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na Mbio za NMB
Bima Marathon zitakazofanyika Jumamosi ijayo. Kushoto ni Mwakilishi wa
waandaaji wa mbio hizo – Baraka Mtavangu na Mwakilishi kutoka Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili – Dkt. Rehema Laiti.
Hizi ndizo jezi zitakazo tumika wakati wa mashindano ya Mbio za NMB Bima Marathon.
Timu ya NMB ikiwa tayari kwa ajili ya Mbio za NMB Bima Marathon.
……………………………………………….
Benki ya NMB inatarajia kukusanya
zaidi ya Sh. milioni 100 kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye saratani
katika mbio za NMB Bima Marathon zilizopangwa kufanyika Septemba 12
jijini Dar es Salaam.
Fedha hizo zinatarajia kupatikana
kupitia kwenye ada ya ushiriki wa mashindano hayo kwa
upande wa Kilometa
5 ambazo zitashirikisha wadau mbalimbali watakaojitokeza kushiriki
katika mbio hizo zilizopangwa kuanzia jengo la Mlimani City.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na
Biashara wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi alisema kuwa
wanatarajia kushirikisha jumla ya wanariadha 3,000 katika mbio hizo
ambazo zimeandaliwa na kampuni ya The Africa Digital Banking Summit
inayoongozwa na Baraka Mtavangu
Mponzi alisema kuwa, viingilio
vyote vya mbio za kilometa 5 vitapelekwa kwenye hospitali ya Muhimbili
kwa ajili ya matibabu ya watoto hao. Alisema kuwa, mbio za kilometa 10
na 21 zitatumika zaidi kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa
bima.
“Tunajisikia fahari kudhamini
mashindano haya kwa ajili ya kusaidia jamii. Tunaomba wadau washiriki
ili kufanikisha lengo au kuzidi lengo hilo. Naomba pia nitoe rai kwa
jamii nzima aidha kushiriki mbio hizi au kuwasajili ndugu na marafiki
ili tuweze kuwagusa watoto wengi zaidi wenye saratani kupata matibabu
hospitali ya Muhimbili,” alisema Mponzi.
Naye, Rehema Laiti ambaye
ni Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili aliwapongeza waandaji wa mbio hizo na zaidi Benki ya NMB kwa
hatua hiyo na kuwataka watu wengine kuiga jambo hilo.
Kwa upande wake Baraka Mtavangu
ambaye ni Mratibu wa NMB Bima Marathon alisema sehemu za kujisajili ni
Mlimani city karibu na KFC pamoja na hospitali ya muhimbili. Wale wote
ambao tayari wameshajisali wanaweza kupata jezi zao hapo hapo Mlimani
city karibia na KFC.
Mbali ya Benki ya NMB, wadhamini
wengine ni kampuni za Bima za Sanlam, Strategies, Reliance na
UAP. Benki hiyo kama mdhamini mkuu imetoa Shilingi milioni 35 kwa ajili
ya udhamini wa mashindano hayo.
No comments :
Post a Comment