Mawakala kutoka Manispaaa ya Temeke wakiwa katika mafunzo ya jinsi wanavyoweza kuzuia utakatishaji fedha
Christine Mwidunda, akitoa mafunzo kwa Mawakala jijini Arusha.
Mawakala wakiwa na vyeti walivyopewa baada ya kuhitimisha mafunzo ya namna gani wanaweza kuzuia utakatishaji fedha.
…………………………………………………………
Benki ya NMB imetoa mafunzo maalum
kwa mawakala wake kuhusiana na namna ya kuzuia utakatishaji fedha; na
pia mbinu za kuzuia kufadhili shughuli za kigaidi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini
Dar es Salaam na Arusha, ni utekelezaji wa maagizo ya
Benki Kuu (BoT)
kuhakikisha mawakala wa benki hawawi sehemu ya kutakatisha fedha
zinazopatikana kwa njia zisizo halali.
Akizungumza wakati wa semina hiyo,
Meneja Mwandamizi wa NMB Kitengo cha Wakala – Bw. James Manyama alisema
ili mawakala hao kutotumika vibaya hawana budi kuzingatia sheria na
kanuni za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ili kushirikiana na Serikali
katika kukomesha vitendo hivyo.
“Ni wajibu wetu kama Benki
kuwaelimisha mawakala wetu kuwa makini wakati wote hasa kwa wateja ambao
wameshajenga ukaribu na mazoea nao. Pia ni muhimu kuwa makini na wateja
wanaoweka fedha nyingi na kisha wanazitoa ndani ya muda mfupi, na
ukiangalia kiasi hicho cha fedha wanachoweka hakiendani na maisha yao.
Inapotokea hali hiyo wanapaswa kutoa taarifa sehemu husika,” alisema James.
Christine Mwidunda, ambaye ni
Meneja wa Mawakala NMB, alisema vyanzo vya fedha haramu ni kama vile
ukwepaji wa kodi, biashara zilizopigwa marufuku zikizemo dawa za
kulevya, usafirishaji wa silaha na binadamu, ugaidi na utekaji n.k.
Katika hatua nyingine Meneja
Wakala wa NMB Kanda ya Kaskazini-Abraham Juma aliwataka Mawakala
kuzingatia taratibu walizopewa zinazowataka wateja wanaoweka na kutoa
fedha kujaza fomu ili kuwa na kumbukumbu ambazo ni matakwa ya BoT.
Mmoja wa Mawakala wa NMB-Monica
Temu alisema mafunzo hayo yamewapa maarifa sahihi ya kuwawezesha
kutekeleza majukumu yao kikamilifu huku wakiwa wanafahamu mipaka ya kazi
na namna ya kutilia mashaka wateja wanaotumia mawakala kutakatisha
fedha zao jambo ambalo pia lingeweza kuwaweka katika wakati mgumu na
mamlaka za nchi.
Benki ya NMB Imepanga kutoa mafunzo haya kwa mawakala wake wote 7700 ambao wametapakaa nchi nzima ifikapo mwezi Oktoba, 2020.
No comments :
Post a Comment