BALOZI
wa Marekani hapa nchini, Dkt. Donald Wright amewataka Watanzania
kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu
ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao
kimaendeleo.
Dkt. Wright amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam ambapo wamejadili
masuala ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Marekani pamoja
na kugusia harakati za kampeni za uchaguzi mkuu unaoendelea hapa
Nchini.
Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amemhakikishia Balozi wa Marekani Dkt.
Wright kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza hususani katika sekta
za utalii,kilimo,na biashara na kumhakikishia kuwa uchaguzi mkuu wa
mwaka huu utakuwa huru,haki na wa amani.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika sekta ya utalii serikali ya awamu
ya tano imedhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na
kupambana na ujangili jambo ambalo limeiwezesha serikali kuanzisha
hifadhi za Taifa mpya nane ikiwa ni pamoja na kuimarisha hatua za
usalama kwa watalii baada ya janga la corona kumalizika nchini.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani hapa Nchini Dkt. Donald Wright
amemhakikishia Waziri kabudi kuwa atahamasisha wafanyabiashara na
wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika sekta za kilimo,biashara,huduma
za afya na viwanda pamoja na kuhamasisha watalii kutoka marekani kuja
nchini.
"Natumia pia fursa hii kuwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua
kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo," Amesema
Dkt. Wright.
No comments :
Post a Comment