Balozi wa Marekani hapa nchini
Mhe. Dkt. Donald Wright akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi wa
Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright moja ya nakala ya kitabu
kinachoelezea masuala ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimkabidhi zawadi ya
picha Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright. Kulia mwa
Waziri ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
*******************************
Balozi wa Marekani hapa nchini
Mhe. Dkt. Donald Wright amewataka Watanzania kushiriki
kikamilifu
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua
kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo.
Dkt. Wright amesema hayo
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini
Dar es Salaam ambapo wamejadili masuala ya ushirikiano wa maendeleo
baina ya Tanzania na Marekani pamoja na kugusia harakati za kampeni za
uchaguzi mkuu unaoendelea hapa Nchini.
Katika mazungumzo hayo Prof.
Kabudi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
amemhakikishia Balozi wa Marekani Dkt. Wright kuwa Tanzania ni sehemu
salama ya kuwekeza hususani katika sekta za utalii,kilimo,na biashara na
kumhakikishia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru,haki na wa
amani.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa
katika sekta ya utalii serikali ya awamu ya tano imedhibiti kwa kiasi
kikubwa uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili jambo
ambalo limeiwezesha serikali kuanzisha hifadhi za Taifa mpya nane ikiwa
ni pamoja na kuimarisha hatua za usalama kwa watalii baada ya janga la
corona kumalizika nchini.
Kwa upande wake Balozi wa
Marekani hapa Nchini Dkt. Donald Wright amemhakikishia Waziri kabudi
kuwa atahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja nchini kuwekeza
katika sekta za kilimo,biashara,huduma za afya na viwanda pamoja na
kuhamasisha watalii kutoka marekani kuja nchini.
“Natumia pia fursa hii
kuwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza
kutekeleza malengo yao kimaendeleo,” Amesema Dkt. Wright.
No comments :
Post a Comment