Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Benny Mwaipaja, akitoa taarifa kwa umma akikanusha taarifa inayosambaa
kwenye mitandao ya kijamii kuwa Wizara ya Fedha na Mipango inashirikiana
na Shirika binafsi la BACC kutoa mitaji ya biashara na kilimo bila riba
wala vikwazo, ofisini kwake jijini Dodoma.
Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
(Picha na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma)
***********************************
Na. Peter Haule na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma
Wizara ya Fedha
na Mipango imekanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii
kuwa inashirikiana na Shirika binafsi la BACC kutoa mitaji ya biashara
na kilimo bila riba
wala vikwazo.
Akiongea jijini
Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, amesema taarifa hiyo ipuuzwe kwa kuwa
Wizara inautaratibu maalumu wa kufikisha taarifa kwa Umma
“Wizara hutumia
njia rasmi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
iliyosajiliwa na kutambulika na Serikali kutoa taarifa zake, hivyo ni
vema kutambua kuwa Wizara haihusiki katika taarifa hizo zenye lengo la
kupotosha umma na kuibua sintofahamu miongoni mwa jamii”, alisema Bw.
Mwaipaja.
Ameitaka jamii kujihadhali na genge hilo la matapeli wanaotumia mitandao ya kijamii kuwarubuni ili kujipatia fedha za wizi.
Alisema kuwa
Wizara haitambui na wala haijawahi kujihusisha kwa namna yoyote na
kampuni hiyo na wala Wizara haina mradi wowote wa namna hiyo wa
kuwakopesha wafanyabiashara na wakulima mikopo isiyo na riba wala
vikwazo.
“Hao ni matapeli wa kimtandao, wapuuzeni”, alisisitiza Bw. Mwaipaja
Aidha, amewaonya
watu wanaofanya vitendo hivyo kuacha maramoja kwani wanatafutwa na
vyombo vya dola kwa udi na uvumba na kwamba wakipatikana hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Bw. Mwaipaja
amewataka wote ambao watapenda kupata maelezo ya ziada kuwasiliana na
Kitengo cha Mawasilaiano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango kupitia
Namba ya simu ya mkononi 075481562.
No comments :
Post a Comment