Kaimu
Mtendaji Mkuu wa OSHA akimsikiliza Balozi wa Heshima wa Seychelles hapa
nchini, Bi. Maryvonne Pool (hayupo pichani), alipotembelewa na Balozi
huyo ofisini kwake. Balozi
wa Heshima wa Seychelles hapa nchini, Bi. Maryvonne Pool, akizungumza
na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alipotembelea ofisi
za OSHA kwa ajili ya kusajili sehemu yake ya kazi na kujifunza namna
ambavyo OSHA inafanya kazi.
************************************
Na Mwandishi Wetu
Balozi wa Heshima wa Seychelles
nchini, Bi. Maryvonne Pool, ameipongeza Tanzania kwa
hatua kubwa
iliyofikiwa katika usimamizi wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi
yenye lengo la kulinda nguvukazi ya Taifa.
Ametoa pongezi hizo leo
alipotembelea ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa
lengo kufanya usajili wa moja ya miradi ambayo ofisi yake ni mbia pamoja
na kujifunza namna ambavyo taasisi ya OSHA inatekeleza majukumu yake.
Bi. Maryvonne Pool amesema
anatambua kazi nzuri inayofanywa na OSHA katika kusimamia utekelezaji
wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo kupitia
sheria hiyo maeneo mengi ya kazi yanatambulika na kuzingatia viwango
vya usalama na afya kazini.
“Naipongeza Tanzania chini ya
uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufili kwa kuwa na taasisi muhimu kama
hii ambayo inasaidia kulinda nguvu kazi ya nchi na kimsingi nimekuwa
nikiwasikia sana siku hizi na nafahamu jinsi mlivyojipanga katika
kutekeleza majukumu yenu ya msingi,” alieza Balozi huyo wa heshima.
Aidha, Balozi huyo ameahidi
kushirikiana na OSHA katika kuviwezesha vikundi vya wakulima wadogo
wanaofanya shughuli zao katika wilaya za pembezoni mwa mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani hususan kuhakikisha kwamba vikundi hivyo vinasajiliwa na
OSHA kwa ajili ya kuendelea kupatiwa miongozo ya namna ya kujikinga na
madhara yatokanayo na shughuli za kilimo.
“Sisi tunafanya miradi mbali mbali
ya kuwawezesha wakulima kuboresha uzalishaji na kupata masoko ya mazao
ya kilimo na japokuwa tumekuwa tukiwawezesha wakulima kupata vifaa
muhimu vya kujikinga kama vile viatu vya shambani (Gunboots) lakini
tunaona ipo haja ya kuwahamasisha wakulima kuwa katika vikundi vya
uzalishaji na kuwawezesha kupata usajili wa OSHA ili muendelee
kuwaongoza kufanya kazi zao kwa usalama zaidi,” alieleza Bi. Maryvonne.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji
Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake imefarijika
kutambua kwamba juhudi za serikali za kulinda nguvukazi ya Taifa
zinaonekana.
“Tumefurahi sana leo kutembelewa
na Balozi wa Heshima wa Seychelles hapa nchini kwetu ambaye amekuja
kusajili eneo lake la kazi. Tumepata fursa ya kushirikishina mambo mengi
na kubadilishana uzoefu jinsi ambavyo nchi zetu zinasimamia masuala ya
afya na usalama ambapo amefurahi sana kuona kwamba nchi yetu ina mfumo
madhubuti wa kusimamia usalama na afya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa,”
alisema Bi. Mwenda.
Katika ziara yake Balozi huyo
alifanikiwa kusajili mradi ambao ofisi yake ni mbia na kupatiwa cheti
cha usajili papo hapo. Aidha, alipata fursa ya kubadilishana uzoefu na
Mtendaji Mkuu wa OSHA kuhusu mifumo ya usimamizi wa masuala ya Usalama
na Afya baina ya Tanzania na Visiwa vya Seychelles ambapo alieleza kuwa
nchi yake ina sheria kali zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali
pa kazi.
Miongoni mwa majukumu ya OSHA ni
kusajili sehemu za kazi na kisha kuendelea kuzitembelea sehemu hizo kwa
ajili ya kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa viwango stahiki vya Usalama
na afya vinavyopaswa kuzingatiwa.
Mwisho……………………
No comments :
Post a Comment