Katibu
Tawala, Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel Kolobelo na Wajumbe wa Kamati ya
Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
*************************************
Na Karimu Meshack; Morogoro
Usimamizi thabiti wa
maadili kwa watumishi wa umma katika kata na vijiji mkoani Morogoro
umetajwa kuwa sababu ya kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Hayo yamesemwa na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel N.M. Kalobelo
alipotembelewa ofini kwake leo na Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani
na Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
Eng. Kalobelo amesema
ukosefu wa maadili kwa watendaji wa kata na vijiji umeonekana kuwa
kichocheo cha migogoro na uvunjifu wa amani katika maeneo mengi nchini
lakini Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli
imefanya kazi kubwa ya kulikomesha tatizo hilo mkoani Morogoro.
“Siku za nyuma Mkoa
wa Morogoro ulikuwa kati ya mikoa yenye migogoro mingi ya ardhi kati ya
wakulima na wafugaji lakini baada ya kufanya utafiti wa kina tukagundua
watendaji na viongozi wa kata na vijiji walikuwa ndiyo chanzo kwani
waliidhinisha uuzaji wa maeneo yasiyopimwa bila kufuata taratibu
sahihi.” Amesema Eng. Kalobelo.
Baada ya kubaini
kinachofanyika na watendaji hao, Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na
wananchi wa maeneo husika tumesimamia kwa nguvu maadili kwa kutumia
mbinu mbalimbali kwa mafanikio na sasa wanafanya kazi zao kiweledi jambo
lililopunguza tatizo kwa kiasi kikubwa.
Aidha Katibu Tawala
huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema wameendelea kushughulikia na kusimamia
upimaji wa ardhi pamoja na ugawaji wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na
kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji kupunguza migogoro ya ardhi
katika mkoa huo na Wilaya zake.
“Kupitia Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tumeanzisha Ofisi ya kusimamia
Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ulisaidia kupima maeneo na kusimamia
ugawaji wake kwa kuyatenganisha ili wakulima wawe na maeneo yao na
wafugaji pia wawe na maeneo yao, mpango huu umesaidia kuzuia muingiliano
wa shughuli za kilimo na ufugaji.” Ameongeza Eng. Kalobelo.
Kamati hii ya Kitaifa
ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliundwa mwezi
Februari, 2012 chini ya Itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari
iliyoridhiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa
Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo (The Pact on Security, Stability
and Development in the Great Lakes Region).
Kamati hiyo
inayoongozwa na Mwenyekiti wake Felistas Mushi wa Wizara ya Katiba na
Sheria inaundwa na Wataalamu wanne ambao ni Miraji Magai Maira wa
Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambaye pia ni Katibu wa Kamati, Saleh Ambika
wa Wizara ya Mambo ya Ndani (Jeshi la Polisi), Lina Kitosi kutoka Ofisi
ya Waziri Mkuu na Pius Katani kutoka Ofisi ya Rais Ikulu.
Kamati hiyo ya
watalaamu watano imefika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuonana na
Katibu Tawala Eng. Emmanuel Kolobelo kabla ya kuelekea Mvomero kukagua
utekelezaji wa masuala ya Ujenzi wa Amani inayohusisha rasilimali na
hatimaye kusababisha mapigano na hata mauaji kati ya wakulima na
wafugaji, wawekezaji na wananchi na wakati mwingine wananchi wenyewe kwa
wenyewe.
No comments :
Post a Comment