Monday, September 7, 2020

JNHPP KUWA INJINI YA UKUAJI UCHUMI WA TANZANIA



*********************************
Na Mwandishi wetu, Rufiji
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani akiwa katika ziara ya kukagu utekelezaji wa Mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) Leo Septemba 7, amesema kuwa
mradi huo unatarajiwa kuwa injini itakayochochea ukuaji wa shughuli za kimaendeleo na uchumi wa Taifa kwa kasi kubwa.
Aliongeza kuwa, Mradi huo wa JNHPP, utazalisha umeme wa bei nafuu wa Jumla ya Megawati 2115 ambazo zitatumika katika shughuli mbalimbali kiuchumi na kimaendeleo na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Utekelezaji wa Mradi huu Mkubwa na wa kimkakati ulianza Mwezi Juni 2019 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022. Lengo la Serikali ni kuhakikisha mradi wa Julius  Nyerere unakamilika ndani ya wakati Alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, Waziri Kalemani aliendelea kwa kueleza kuwa, kulingana na mpango kazi uliopo, Serikali ya Tanzania imeshamlipa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo zaidi shilingi trilioni 1.49 ambayo ni sawa na asilimia 22 ya malipo yote ya mradi.
Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali tayari imetenga kiasi cha Shilingi za Tanzania Trilioni 1.44 kwaajili ya kuendeleza shughuli za Mradi wa huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani, mradi wa JNHPP utakuwa ni kama injini ya uchumi wa Tanzania, kwani kukamilika kwake kunatarajiwa kushusha bei ya umeme na kukuza uwekezaji hasa sekta ya viwanda nchini itakayozalisha ajira pamoja na kuongeza vipato vya wananchi pamoja na pato la Taifa.
Mradi wa Julius Nyerere unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani ambazo ni kiasi cha shilingi trilioni 6.558 mpaka kukamilika kwake.
Mradi huu pia, utasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza ukataji wa miti kutokana na kushuka kwa gharama za umeme.
Aliongeza kuwa, mradi wa JNHPP ndio utakao tatua matatizo ya umeme nchini hivyo kukamilika kwake kuna tija kubwa sana kwa Taifa na Mwananchi mmoja mmoja kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliambatana Naibu Waziri wa Ujenzi Misri Mhandisi Jenerali Mohmoud Nassar, Katibu Mkuu Nishati Mhandisi Zena Said, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi, Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Dkt. Tito Mwinuka na Naibu Mkurugenzi Uwekezaji TANESCO Mhandisi Khalid James.

No comments :

Post a Comment