Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi (kulia) akizungumza kwenye hafla ya tuzo na semina ya wanahabari iliyoandaliwa na TMA. |
Ofisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni akielezea mchakato wa tuzo hizo kabla ya washindi kutangazwa. |
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) imetoa tuzo kwa wanahabari bora wa uandishi wa habari za
Hali ya Hewa nchini kwa mwaka 2020. Wanahabari watatu wamebahatika
kushinda
tuzo hizo zilizotolewa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo wakati akikabidhi
tuzo hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA), Dk. Buruhani Nyenzi alisema TMA inatambua mchango mkubwa wa
wanahabari katika kuhabarisha umma juu ya taarifa za mamlaka hiyo na
ndio maana imeanza kutoa motisha kwao.
Mwanahabari alieibuka mshindi wa
kwanza ni Bi. Theopista Nsanzugwako kutoka Gazeti la Habari Leo, na Bw.
Jerome Risasi kutoka Clouds Media kushika nafasi ya pili, huku nafasi ya
tatu ikinyakuliwa na Bw. Daniel Samson mwandishi wa habari kutoka
Mtandao wa Nukta.
Aidha Dk. Nyenzi aliwataka
wanahabari walioshinda kutumia tuzo hizo kama chachu ya kuongeza umahiri
na uandishi wa habari za hali ya hewa, na wale ambao hawakushinda
safari hii kuongeza bidii ili kuleta ushindani zaidi katika tuzo zijazo.
Amesema TMA itaendelea
kuziboresha tuzo hizo na kuwaomba wanahabari kujitokeza zaidi katika
shindano lijalo ambalo muda ukifika litatangazwa tena. Awali akitangaza
namna washindi walivyopatikana katika mchuano huo, Ofisa Uhusiano wa
TMA, Monica Mutoni alisema timu ya majaji wa tuzo hizo ilitangaza muda
wa kupokea kazi za wanahabari kabla ya kuzichakata na kuibuka na
washindi.
Utoaji wa tuzo hizo leo ulienda
sambamba na warsha ya wanahabari, kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za
vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2020 nchini, iliyofanyika
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Ubungo
Plaza, Dar es Salaam
No comments :
Post a Comment