Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (katikati) akiongea na waandishi
wa habari leo jijini Mwanza kutangaza uamuzi wa kuanza kuwalipa
wakulima wa kahawa wa mkoa wa Kagera fedha zao shilingi Bilioni 12
kupitia Vyama Vikuu vya KDCU na KCU.Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda na Biashara Prof.Riziki Shemdoe. Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu
Wizara ya Viwanda na Biashara Prof.Riziki Shemdoe (kulia) wakati wa
kikao kilichojadili ulipwaji wa madeni ya wakulima wa zao la kahawa kwa
vyama vikuu vya ushirika KDCU na KCU utakaonza kesho .Kikao kimefanyika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.Picha
ya pamoja kati ya Makatibu Wakuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( wa
pili kushoto) akiwa kwenye kikao leo Mwanza kujadili kuanza kulipwa
kwa wakulima wa Kahawa Kagera.Wengine ni Bw.Emanuel Tutupa (RAS Mwanza)
katikati,Prof.Riziki Shemdoe ( Katibu Mkuu Viwanda) na Prof.Faustin
Kamuzola (RAS Kagera aliyevaa kofia).
************************************
Serikali imesema wakulima
waliokusanya kahawa yao kwenye vyama vya ushirika mkoani Kagera wataanza
kulipwa madeni yao mapema wiki hii.
Kauli hiyo imetolewa leo
(01.09.2020) Jijini Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald
Kusaya wakati alipoongoza kikao cha viongozi wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, mikoa ya Mwanza na Kagera na vyama vikuu vya Ushirika KDCU na
KCU kilichofanyika
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kusaya alisema tangu msimu wa
ununuzi wa kahawa ulipofunguliwa mwezi Juni mwaka huu jumla ya shilingi
Biioni 32 tayari zimelipwa kwa wakulima wa mkoa wa Kagera kutokana na
kukusanya tani 62,336 za kahawa ghafi na tani 31,168 za kahawa safi
kwenye vyama vikuu vya ushirika na vile vya msingi.
“Pamoja na kulipa Bilioni 32 za
wakulima bado Chama Kikuu cha Ushirika KDCU kinadaiwa shilingi Bilioni
12 kutokana na kukusanya kahawa ya wakulima ,hivyo kikao chetu leo
tumekubaliana KDCU waanze kulipa wakulima shilingi Bilioni 7 zilizopo
tayari kuanzia kesho na zingine Bilioni 5 zitalipwa mapema wiki ijayo”
alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo alisema deni hilo
linatokana na KDCU kuendelea kukusanya kahawa ya wakulima kufuatia
uwepo wa mavuno mazuri ambapo takwimu zinaonesha wanakusanya kwa siku
kahawa yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.7 kutoka kwa wakulima na
tayari wamenunua kilo milioni 37.3 kati ya lengo la kilo milioni 45 za
kahawa msimu huu.
Kuhusu Chama Kikuu cha Kagera (
KCU) ,Katibu Mkuu Kusaya alisema wanadaiwa na wakulima shilingi Bilioni
7.1 na kuwa wamekubaliana kuanza kulipa shilingi Bilioni 2 mapema wiki
huku wakiendelea na kukusanya fedha toka kwa wanunuzi waliowauzia
kahawa.
“Shilingi Bilioni 2 za wakulima
waliouza kahawa KCU tumekubaliana zitaanza kulipwa wiki hii Kagera na
kuwa zingine Bilioni 3 zitatolewa na mnunuzi aliyeuziwa kahawa na KCU
katika muda mfupi ujao” alisisitiza Kusaya.
Kusaya aliongeza kusema serikali
imejipanga kikamilifu kuona wakulima wa kahawa kote nchini wanalipwa
fedha zao kwani mfumo unaotumika wa vyama vikuu na AMCOS kununulia
kahawa ni wa uhakika na kuwa wakulima wawe na subira kipindi kifupi
fedha zitapatikana kwani wanunuzi toka nje ya nchi wameanza kuonyesha
nia ya kuja Tanzania kutokana na tatizo la korona kudhibitiwa .
“Kuchelewa kwa malipo ya wakulima
wa kahawa hususan mkoa wa Kagera yametokana na vyama vikuu vya ushirika
kuchelewa kuuza kahawa” alisema Kusaya na kuwa serikali ipo tayari
kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa mikopo kwa vyama vya
ushirika kununua kahawa na kulipa wakulima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe alisema kwa
kushirikiana na Wizara ya Kilimo wanaendelea kutafuta masoko ya uhakika
ya mazao ya wakulima kama alivyoelekeza Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
Prof. Shemdoe alisema kwa sasa
wanunuzi na wafanyabiashara binafsi wanaruhusiwa kununua kahawa toka
vyama vikuu vya ushirika au vyama vya msingi (AMCOS) lakini wahakikishe
wanatoa bei nzuri na yenye ushindani wa soko.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa
wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora alisema wakulima wa kahawa msimu huu
wamepata bei nzuri karibu asilimia 75 ya bei ya soko la dunia na kuwa
vyama vikuu vya Ushirika (KDCU) na (KCU) kwa mkoa wa Kagera wamefanya
kazi nzuri kuwezesha wakulima kulipwa bei nzuri.
Prof.Kamuzora ametoa wito kwa
watanzania kuwa na tabia ya kunywa kahawa ili kusaidia upatikanaji wa
soko la kahawa ndani ya nchi tofauti na ilivyo sasa kahawa asilimia 93
inayozalishwa nchini inauzwa nje ya nchi.
Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya
Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege alisema wanunuzi binafsi wa kahawa
wanaruhusiwa kununua lakini sharti waingie mikataba na vyama vya vikuu
vya ushirika au AMCOS ili kuwa na uhakika wa bei nzuri kumfikia mkulima.
Dkt. Ndiege alitoa wito kwa
viongozi wa vyama vya ushirika nchini hususan mkoa wa Kagera kutoa
kipaumbele cha malipo ya wakulima waliouza mapema kahawa yao kutokana na
fedha zilizopatikana sasa na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha
Makatibu Wakuu Kilimo na Viwanda .
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya
Kahawa Tanzania imeonesha makusanyo ya kahawa msimu wa 2020/2021
yamefikia jumla ya tani 79,245 (73%) za kahawa ghafi kati ya lengo la
tani 108,000 na tani 44,695 (63 %) za kahawa safi kati ya lengo la tani
70,000.
Kahawa hiyo imekusanywa toka kwenye mikoa yote 17 inayolima zao la kahawa nchini.
Aidha bei ya kahawa kwa mkulima
msimu huu imekuwa ikilipwa kwa utaratibu wa malipo ya awali kupitia
vyama vyao vya ushirika ambapo mkulima analipwa kwa kilo shilingi 1,200
kahawa ya Robusta maganda (dry cherry) na shilingi 1,250 na 1,500 kahawa
za Arabika maganda (parchment)
No comments :
Post a Comment